Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

BRELA NA NHIF WAJADILI UBORESHAJI WA HUDUMA ZA AFYA KWA WATUMISHI


Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, leo tarehe 12 Mei 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Ilala, yakilenga kuboresha huduma za afya kwa watumishi wa Wakala.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi Kuu za taasisi hiyo, Bw. Nyaisa alisisitiza kuwa ustawi wa wafanyakazi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, sambamba na kuendana na dira ya taasisi.

“Afya ya mtumishi ni msingi mkuu wa ufanisi wa taasisi katika kuwahudumia wananchi, hivyo ni muhimu watumishi kuwa na uhakika wa kupata huduma bora za afya,” alisema Bw. Nyaisa.

Kwa upande wake, Meneja wa NHIF Mkoa wa Ilala, Aifena Mramba, alisema kikao hicho kimekuwa na tija kubwa na kimefungua fursa ya kushughulikia changamoto za watumishi kwa haraka zaidi.

Aidha, alieleza kuridhishwa na ushirikiano uliopo kutoka kwa uongozi wa juu wa BRELA, akibainisha kuwa NHIF inaendelea kuimarisha mifumo ya kidigitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama wake.

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji kutoka BRELA, Lameck Kabeho, alisema pande zote mbili zimejadili kwa kina namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili watumishi wanapohitaji huduma za afya katika vituo vya tiba.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa mtumishi wa BRELA pamoja na wategemezi wake wanapata huduma stahiki kwa wakati, bila usumbufu wowote,” alisema Bw. Kabeho.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za BRELA kuendelea kuboresha ustawi wa watumishi wake kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za matibabu kupitia NHIF bila vikwazo, hatua inayochochea ufanisi wa kazi.