Habari
VIJANA WAHIMIZWA KUTUMIA UBUNIFU NA TEKNOLOJIA KUKUZA BIASHARA
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. William Trachman, amewahimiza vijana wajasiriamali kuwekeza katika ubunifu, kuimarisha mitandao ya kibiashara na kutumia fursa za ushirikiano wa kimataifa ili kukuza biashara zao na kuvutia wawekezaji.
Akizungumza katika Kongamano la Biashara Bunifu lililofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 21 2026 katika kituo Cha mikutano Cha Julius Nyerere amesema, “mafanikio ya biashara yanahitaji juhudi, uvumilivu na uwezo wa kubuni bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya soko”.
Balozi Tracham, alisisitiza kuwa mazingira rafiki ya biashara, sera zinazoeleweka na uhakika wa kisheria ni muhimu katika kujenga imani kwa wawekezaji na kuvutia mitaji ya muda mrefu.
Aidha, amewahimiza vijana kutumia teknolojia ili kutatua changamoto katika jamii, kujifunza kutokana na mabadiliko ya soko na kufanya maamuzi yenye ujasiri ili kujenga biashara endelevu na zenye ushindani.
Kongamano hilo liliwakutanisha vijana mbalimbali wenye biashara changa na bunifu kwa lengo la kuwapatia maarifa, kubadilishana uzoefu, kuimarisha mitandao ya kibiashara na kuwafungulia fursa za ushirikiano na uwekezaji zitakazochochea ukuaji wa biashara zao.
