Habari
WAFANYABIASHARA WA MTANDAONI LINDENI NEMBO ZETU
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amewataka wajasiriamali wanaofanya biashara kupitia mitandao ya kijamii kusajili na kulinda nembo zao kisheria kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwani kuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii pekee hakutoshi kuhakikisha ulinzi wa nembo ya biashara yako.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo Oktoba 21, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Jukwaa la CRDB INSTAPRENYUA 2026 lililoandaliwa na Benki ya CRDB, ambapo alieleza kuwa biashara za mtandaoni zimekuwa fursa muhimu kwa wajasiriamali kuwafikia wateja wengi na masoko mbalimbali bila kuhitaji eneo maalumu la kufanyia biashara.
Aidha, alisisitiza kuwa wajasiriamali wanapaswa kutumia fursa hiyo kusajili nembo zao kupitia BRELA ili kupata ulinzi wa kisheria na kulinda uwekezaji, muda na juhudi walizoweka katika kuanzisha na kukuza biashara zao. Pia alieleza huduma za BRELA zinapatikana kwa njia ya kidijitali, hivyo wajasiriamali wanaweza kusajili nembo zao bila kulazimika kufika ofisini.
“Ili uweze kutetea nembo yako, lazima uisajili BRELA kwa hiyo, lindeni nembo zenu kupitia sheria zetu za nchi. BRELA wanafanya huduma hizi kidijitali, hakuna haja ya kufika ofisini. Sajilini nembo zenu kwa sababu mmetumia nguvu kubwa sana kuzianzisha, kwa hiyo mtumie nguvu hiyo hiyo kuzilinda,” amesema Mhe. Kapinga.
BRELA imeshiriki katika Jukwaa la CRDB INSTAPRENYUA 2026 lililofanyika kwa siku mbili, kuanzia Oktoba 21 hadi 22, 2026, jijini Dar es Salaam, kwa kutoa elimu kuhusu urasimishaji wa biashara na ulinzi wa alama za biashara kwa wajasiriamali.
