Habari
WAHITIMU WA MZUMBE WATAKIWA KUWA KICHOCHEO CHA UTEKELEZAJI WA DIRA 2050
Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe wametakiwa kuwa kichocheo cha utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 kwa kutumia maarifa, ujuzi na ubunifu walioupata chuoni hapo.
Hayo yamebainishwa wakati wa Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe (26th AGM of the Mzumbe University Convocation), ambapo BRELA ilitoa tuzo kwa mhitimu bora wa chuo hicho, Bw. Colins David Mulemwa, aliyepata GPA ya 4.7 katika Shahada ya Kwanza ya Uhasibu na Fedha.
Awali, akizungumza katika mkutano huo uliofanyika tarehe 21 Oktoba 2026 Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu iliyopo mkoani Morogoro, mgeni rasmi ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mstaafu Prof. Elisante Ole Gabriel, alisema wahitimu wana nafasi muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 endapo watatumia ipasavyo maarifa na ujuzi walioupata katika elimu yao.
“Chuo hiki kimezalisha wataalamu mbalimbali wanaofanya vizuri katika sekta binafsi na ya umma. Hivyo, ni muhimu kwa wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata chuoni kuwa kichocheo cha kuiwezesha nchi kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa haraka,” alisema Prof. Ole Gabriel.
Kwa upande wake, Bw. Nehemia Mihayo, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, alisema ushiriki wa BRELA katika mkutano huo ulilenga kuwahamasisha vijana kufanya vizuri katika masomo yao na kuwapatia elimu kuhusu taratibu sahihi za kuanzisha na kuendesha biashara.
“Elimu ni ufunguo wa maisha na BRELA ni lango la mafanikio ya biashara, hivyo tunafungamanisha mambo haya mawili kwa kutambua kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inasisitiza ubunifu, ujasiriamali na maendeleo ya biashara ndogo na za kati,” alisema Bw. Mihayo.
Aidha, aliongeza kuwa BRELA inatoa huduma mbalimbali zinazohusiana na urasimishaji na uendelezaji wa biashara, zikiwemo usajili wa kampuni, usajili wa majina ya biashara, usajili wa alama za biashara na huduma, utoaji wa hataza, utoaji wa leseni za biashara za kundi A na leseni za viwanda.
Alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuzifahamu na kuzitumia huduma hizo ili kurasimisha shughuli zao za kibiashara na kuendesha biashara zao kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
“Serikali si chanzo pekee cha ajira kwa vijana. Kuna fursa nyingi, zikiwemo zabuni za serikali zilizotengwa kwa ajili ya vijana, mikopo kwa vikundi na fursa nyingine za kiuchumi. Hata hivyo, baadhi ya vijana wanashindwa kuzifikia fursa hizi kwa sababu hawajarasimisha biashara zao. Hivyo, ni wajibu wetu kama taasisi kutoa elimu itakayowawezesha vijana kufuata taratibu sahihi na kunufaika na fursa zilizopo,” alisema Bw. Mihayo.
Kwa upande mwingine, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. William Mwegoha, aliishukuru BRELA kwa kushirikiana na chuo hicho na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo. Alisisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha elimu inayotolewa chuoni hapo ina ubora na inaleta tija kwa jamii, kwa kuzingatia mahitaji ya mazingira yaliyopo.
Ushirikiano kati ya BRELA na Chuo Kikuu cha Mzumbe unalenga kuimarisha uelewa wa vijana kuhusu fursa za biashara, ujasiriamali na urasimishaji wa biashara, ili kuwawezesha kutumia elimu yao kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kufanikisha malengo ya taifa ya muda mrefu.
