Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

BRELA KUANZISHA MADAWATI YA MILIKI UBUNIFU NCHI NZIMA


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imekusudia kuanzisha madawati ya Miliki Ubunifu katika Vyuo vya Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti nchini kwa kushirikiana na Taasisi hizo kwa lengo la kusimamia na kulinda na bunifu zinazozalishwa ndani ya Taasisi hizo.

Mpango huo umeelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau kuhusu uanzishwaji wa Madawati hayo, kilichofanyika Septemba 8, 2025 Jijini Dar es Salaam.

Bw. Nyaisa amesema kuwa bunifu zinazozalishwa na vyuo na taasisi za utafiti zinapaswa kutazamwa kama bidhaa na huduma zenye thamani, zenye uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali katika jamii. 

Ameeleza kuwa, ni muhimu bunifu hizo kulindwa kisheria kupitia Hataza na aina nyingine za Miliki Ubunifu, ili ziweze kuwanufaisha wabunifu, vyuo husika, na jamii kwa ujumla.

“Tunatarajia kuona vyuo vikianzisha kampuni za ubunifu (spin-out companies), kuibua masuluhisho ya changamoto za kijamii, kuongeza ajira na kipato kwa wabunifu na watafiti, pamoja na kuchochea ukuaji wa teknolojia na uchumi,” amesema Bw. Nyaisa.

Bw. Nyaisa ameongeza kuwa, kwa kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2020, BRELA imepokea jumla ya maombi 81 ya Hataza kutoka vyuo vikuu mbalimbali. Kati ya maombi hayo, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela pekee imewasilisha jumla ya maombi 41. Imesema idadi ya Hataza zinazotoka Vyuoni ndogo sana, hivyo kuvitaka vyuo na tasisi nyingine kuongeza jitihada katika kufanya Tafiti zinazolenga kutoa masuluhisho ya kiteknolojia katika Jamii na kuongeza idadi ya  maombi ya Hataza kutoka katika Vyuo hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Bi. Loy Mhando, amesema kikao hicho ni hatua muhimu katika kuunganisha mnyororo wa thamani kati ya utafiti, ubunifu, na miliki ubunifu.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wengine wa mafunzo hayo,  Dkt. Kijakazi Mashoto, Mtafiti Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha …kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), amesema kuwa huu ni wakati muafaka kwa vyuo vikuu na taasisi zilizo kwenye mnyororo wa thamani wa ubunifu, kujifunza jinsi ya kuunganisha matokeo ya tafiti na mahitaji ya soko.

“Semina hii itanisaidia zaidi kuishauri Taasisi yangu kuhusu namna gani matokeo ya tafiti zetu yanaweza kulindwa na kubadilishwa kuwa bunifu zenye uwezo wa kuingia sokoni,” amesema Dkt. Mashoto.

Naye, Dkt. Erasto Mlyuka, Meneja wa Usimamizi na Uhawilishaji wa Teknolojia kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ameipongeza BRELA kwa juhudi zake za kipekee za kuwaunganisha wadau wa Miliki Ubunifu na kuwajengea uelewa juu ya namna ya kuzilinda na kuziendeleza kuwa bidhaa zenye thamani ya kiuchumi.

Kikao hicho cha siku mbili kinahusisha wadau kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wawakilishi kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti, na wataalamu wa sekta ya Miliki Ubunifu.