Habari
WAZIRI AIPONGEZA BRELA KWA KUBORESHA MIFUMO NA KUONGEZA UFANISI
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga, ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa hatua kubwa za kuboresha mifumo ya utoaji huduma ili kuendana na dira ya Serikali katika masuala ya Biashara na Uwekezaji.
Akizungumza katika ziara yake aliyoifanya kwenye ofisi za BRELA, leo tarehe 27 Novemba 2025 Mhe. Kapinga alisema Serikali inaendelea kushuhudia mapinduzi makubwa ya kiteknolojia kwenye sekta ya viwanda, hivyo ni muhimu taasisi zinazohusiana moja kwa moja na biashara kuendelea kuboresha huduma zake.
“Tuko kwenye mapinduzi makubwa ya kiteknolojia, katika kipindi kama hiki huwezi kuacha kuzungumzia teknolojia inayorahisisha mazingira ya kufanya biashara. Nawapongeza kwa maboresho makubwa ya mifumo ambayo imeleta tija kwa kiasi kikubwa,” alisema Waziri Mhe. Kapinga
Aidha, alieleza kuwa mpango wa maendeleo wa nchi unakusudia kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa trilioni dola na kwamba hilo linawezekana kwa kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara, kupunguza gharama na muda wa kuanzisha na kuendesha biashara, pamoja na kuwa na taasisi za umma zenye ufanisi na mifumo ya kidijitali inayounganishwa kikamilifu.
“Ninaamini BRELA ni lango kuu la kuingia kwenye uchumi wa soko, ndiyo mlango wa kwanza wa usajili wa makampuni, majina ya biashara, na mlinzi wa haki za miliki bunifu, alama za biashara na miundo bunifu ya viwandani,” alieleza Mhe. Kapinga
Katika miaka hii mitano, matarajio ya Rais ni makubwa sana, ameahidi ajira milioni nane, mitaa ya viwanda kila wilaya na fedha za mfuko wa vijana kwa ajili ya kuchochea ajira, hatua zote hizi chanzo chake ni hapa BRELA.
Vile vile Waziri Kapinga aliongeza kuwa mafanikio ya uwekezaji yamejikita katika namna taasisi kama BRELA zinavyorahisisha taratibu za biashara na kusisitiza kuwa dira ya mwaka 2050 inalenga mafanikio ambayo Serikali inaamini yanaweza kufikiwa kwa kuwekeza kwenye ubunifu, sekta binafsi na teknolojia.
