Habari
BRELA KUFANYWA CHOMBO IMARA CHA SERIKALI KATIKA KUTOA HUDUMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa mafanikio makubwa iliyoyapata na kusisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kuifanya kuwa chombo imara cha Serikali katika utoaji wa huduma.
Dkt. Abdallah ameyasema hayo leo, tarehe 19 Septemba 2025, alipofungua kikao cha kwanza cha Baraza la Wafanyakazi kwa mwaka wa fedha 2025/26 kinachofanyika jijini Arusha.
Akiwasilisha hotuba yake, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita BRELA imefanya mambo makubwa yanayounga mkono jitihada za Serikali.
“Naomba niwahakikishie kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nanyi bega kwa bega ili kuhakikisha BRELA inaendelea kuwa chombo imara cha Serikali katika kutoa huduma bora, zenye ufanisi, na zinazochangia kukuza biashara na uwekezaji nchini,” alisema Dkt. Abdallah.
Aidha, ameitaka BRELA kutumia Baraza hilo kuimarisha mshikamano na ushirikiano ili kusaidia Wizara na taifa kwa ujumla katika kufanikisha mageuzi ya kiuchumi.
“Nchi yetu ipo katika kipindi cha mageuzi makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia. Ili kufanikisha hili, tunahitaji mshikamano thabiti kati ya mwajiri na wafanyakazi, mshikamano unaojengwa juu ya msingi wa kuheshimiana, kushirikiana, na kutimiza wajibu wa kila upande,” aliongeza Dkt. Abdallah.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya BRELA, Profesa Neema Mori, amesema kuwa Bodi itaendelea kutoa miongozo sahihi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakala pamoja na kutoa ushauri kwa Waziri kuhusu namna bora ya kuboresha utendaji wake.
Awali, akitoa neno la ukaribisho, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 taasisi imefanikiwa kufikia malengo yake ya makusanyo na utekelezaji kwa kiwango cha juu.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wakala umefanikiwa kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa kufikia zaidi ya asilimia 115 ya lengo lililowekwa, na kwa wastani tumetekeleza malengo kwa zaidi ya asilimia 110. Mafanikio haya yametokana na mshikamano, bidii, na kujituma kwa wafanyakazi wote wa BRELA,” alisema Bw. Nyaisa.
Kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha siku mbili kinachofanyika tarehe 19 na 20 Septemba 2025 jijini Arusha, kitajadili pamoja na mambo mengine Taarifa ya Utendaji wa Wakala kwa mwaka wa fedha 2024/25 na Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wakala (2021/2022–2025/2026) kwa kipindi cha miaka minne.