Habari
BRELA KUFUNGUA LANGO LA MAFANIKIO YA SEKTA YA UTALII
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeweka dhamira ya kufungua na kuimarisha milango ya mafanikio katika sekta ya utalii nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 20 Novemba 2025 jijini Arusha na Afisa Leseni wa BRELA, Bw. Koyan Aboubakari, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu, Bw. Godfrey Nyaisa, katika Mkutano wa 42 wa Mwaka wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Utalii Tanzania (TATO).
Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Aboubakari ameeleza kuwa sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, hivyo BRELA ina sababu ya msingi kuhakikisha sekta hiyo inafikiwa na kuimarishwa kupitia urasimishaji endelevu wa biashara.
“Ripoti za mwaka wa fedha 2024/25 zinaonesha kuwa mapato ya sekta ya utalii yameongezeka kutoka TZS bilioni 377 mwaka 2020 hadi TZS bilioni 877 kufikia Machi 2025. Takwimu hizi zinatupa hamasa kubwa ya kuifikia sekta hii ili kuimarisha mazingira ya kufanya biashara,” amesema Bw. Aboubakari.
Ameeleza kuwa kupitia ushiriki wa BRELA katika mkutano huo, wanachama wa TATO zaidi ya 400 wamepata fursa ya kuwasilisha changamoto zao na kupata majibu, ufafanuzi na elimu ya papo kwa hapo kutoka BRELA.
Aidha, amesema kuwa lengo la BRELA kwa sasa ni kuhakikisha inawafikia wadau kupitia miavuli yao ya kibiashara kwa kuendelea kutoa elimu, kutatua changamoto na kupunguza urasimu katika huduma za urasimishaji.
“Dira ya BRELA ni kuweka mazingira wezeshi ya biashara ili kumwezesha kila Mtanzania kuanzisha biashara kwa urahisi bila usumbufu na milolongo isiyo ya lazima,” amesisitiza Bw. Aboubakari.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa wadau na umma kwa ujumla kuwa na mtazamo chanya kuhusu urasimishaji wa biashara, akisisitiza kuwa huduma za BRELA hazilengi wafanyabiashara wakubwa pekee bali zinawahudumia pia wajasiriamali na wafanyabiashara wa ngazi zote.
Mathalani Usajili wa Jina la Biashara ni Shilingi elfu ishirini tu (20,000) Usajili wa Kampuni kwa kiwango cha chini ada ya Usajili ni Laki moja na elfu sitini na saba na mia mbili (167,000) na Usajili wa Kiwanda chenye kiasi cha uwekezaji usiozidi Milioni tano (5,000,000) ni elfu kumi (10,000)” ameeleza Bw. Aboubakari.
