Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

BRELA KUVUTIA MIRADI YA KUKUZA UBUNIFU KUPITIA ARIPO


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imelenga kutumia Mkutano Mkuu wa 49 wa Baraza la Utawala la Shirika la Miliki Ubunifu la Kanda ya Afrika (ARIPO) kama jukwaa la kuvutia miradi ya kukuza sekta ya ubunifu nchini Tanzania.

Hayo yameelezwa jijini Accra, Ghana, tarehe 17 Novemba 2025 na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, wakati akishiriki mkutano huo unaojadili Mpango Kazi na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026.

Bw. Nyaisa amesema kuwa Baraza la Utawala linajadili na kupitisha Taarifa ya Mwaka ya ARIPO, ikiwa ni pamoja na tathmini ya shughuli zilizotekelezwa, mafanikio, changamoto na maeneo ya kipaumbele kwa mwaka ujao.

“Mkutano huu ni muhimu kwa Tanzania, na BRELA imebeba ajenda ya kitaifa kuhakikisha kuwa kupitia Baraza hili tunavutia na kutenga rasilimali kwa ajili ya kuendeleza miradi ya sekta ya miliki ubunifu, ikiwemo miradi inayoendelea na mipya itakayosaidia kuimarisha mifumo ya miliki ubunifu nchini,” amesema Bw. Nyaisa.

Aidha, mkutano huo unajadili na kuandaa nyaraka mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri la ARIPO litakalofanyika tarehe 21–22 Novemba 2025, pia jijini Accra. Baraza la Mawaziri ndilo chombo cha juu kinachotoa maamuzi ya sera na mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za ARIPO.

Vilevile, Kikao cha Baraza la Utawala kinapitia na kuridhia Mpango Kazi na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026 ambayo itaongoza utekelezaji wa programu na mikakati ya kuimarisha mifumo ya miliki ubunifu katika ukanda wa Afrika.

Katika mkutano huo, ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, akiambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi Nyari.

Mkutano huo unaofanyika jijini Accra kuanzia tarehe 17–20 Novemba 2025, umefunguliwa rasmi na Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria wa Ghana, Mhe. Dkt. Dominic Akuritinga Ayine, na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi wanachama wa ARIPO.

Baraza la Utawala ni jukwaa muhimu la kupanga mwelekeo wa taasisi hiyo, hususan katika usimamizi wa haki za miliki ubunifu na kuongeza mchango wa ubunifu katika maendeleo ya uchumi wa Afrika.

Ushiriki wa Tanzania kupitia BRELA na Wizara ya Viwanda na Biashara unaonesha dhamira ya nchi katika kuchochea ubunifu, kuimarisha ulinzi wa haki za wabunifu, na kuongeza mchango wa miliki ubunifu katika kukuza biashara, viwanda na uwekezaji kwa kushirikiana na ARIPO.

Tanzania inaendelea kujenga mazingira wezeshi ya biashara na kuhamasisha ubunifu unaolinda bidhaa na huduma za wazalendo katika soko la kikanda na kimataifa.