Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA na URSB Kuwezesha Huduma za Kidijitali


BRELA na URSB Kuwezesha Huduma za Kidijitali

Katika hatua ya kihistoria inayolenga kuimarisha huduma za kisasa kwa wananchi na wafanyabiashara wa Afrika Mashariki, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umefanya kikao kazi na Ofisi ya Huduma za Usajili Uganda (URSB) kwa lengo la kuweka misingi ya ushirikiano wa karibu katika kuboresha huduma za kidijitali.

 

Kikao hicho kilifanyika  katika ofisi za BRELA, jijini Dar es Salaam, kikiwakutanisha viongozi wa juu kutoka taasisi hizo mbili. Mazungumzo hayo yalilenga kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za kiutendaji, ikiwa ni sehemu ya jitihada za pamoja kuongeza ufanisi na urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa njia ya mtandao.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, alieleza kuwa BRELA inaendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya kidijitali inayorahisisha huduma kwa wananchi. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda ili kuongeza thamani ya huduma zinazotolewa na taasisi hizo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

 

“Ni muhimu kwa taasisi zetu kushirikiana katika maeneo ya msingi kama vile usajili wa kampuni, miliki ubunifu na mifumo ya TEHAMA. Ushirikiano huu utawezesha huduma kufikika kwa urahisi zaidi na kuongeza tija kwa pande zote mbili,” alisema Bw. Nyaisa.

 

Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa URSB, Bi. Mercy Kainobwisho, aliipongeza BRELA kwa hatua kubwa ilizopiga katika mabadiliko ya utoaji huduma kwa njia ya mtandao. Alieleza kuwa URSB ipo tayari kushirikiana kwa karibu na BRELA katika maeneo mbalimbali ya utendaji ili kuboresha huduma kwa wananchi wa Uganda na Tanzania.

 

“BRELA imeonesha mfano bora wa mabadiliko ya kidijitali. Kupitia ushirikiano huu, tunatarajia kujifunza zaidi, kubadilishana uzoefu na kuimarisha huduma zetu kwa wananchi,” alisema Bi. Mercy.

 

Alitaja maeneo ya usajili wa biashara, ubunifu wa miliki namatumizi ya TEHAMA kuwa miongoni mwa fursa muhimu za kushirikiana na kuongeza ufanisi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

Ushirikiano huu mpya kati ya BRELA na URSB unatarajiwa kuwa chachu ya mapinduzi ya kidijitali katika utoaji wa huduma, na kuchochea ukuaji wa biashara na ubunifu katika ukanda huu kwa kutumia teknolojia kama msingi wa maendeleo endelevu.