Habari
BRELA YAENDESHA KIKAO CHA KUPOKEA MAONI KUHUSU ITIFAKI ZINAZOSIMAMIWA NA ARIPO NA WIPO
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imefanya kikao maalum cha wadau kujadili na kupokea maoni ya hatua za awali za mapendekezo ya uridhiwaji wa Itifaki nne za Miliki Ubunifu zinazosimamiwa na ARIPO pamoja na WIPO.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washiriki kutoka Wizara mbalimbali, Taasisi za Serikali pamoja na Sekta binafsi.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kikao hicho, kilichofanyika tarehe 26, Novemba 2025, Bw. Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA alisema kuwa, uridhiwaji wa Itifaki hizo utaiwezesha Tanzania kuimarisha ulinzi wa haki za Miliki Ubunifu ili kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma kimataifa hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Mchango wenu leo unaweka msingi wa mustakabali wa Miliki Ubunifu nchini, mmeacha majukumu yenu na kuja kuandika historia ya kujenga mfumo imara utakaowanufaisha wabunifu, wafanyabiashara, watafiti na vijana wetu,” alisema Bw. Nyaisa
Aidha, Bw. Nyaisa alibainisha kuwa katika dunia ya sasa Miliki Ubunifu ni injini ya uchumi wa sasa na kupitia uimarishaji wa mifumo, kufungua milango ya uwekezaji kutawasaidia wabunifu kulinda kazi zao na kunajenga Taifa lenye ushindani wa kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Bi. Loy Mhando, alibainisha kuwa kikao hicho ni hatua muhimu katika mchakato wa kuhakikisha Tanzania inaenda sambamba na mabadiliko yanayotokea duniani hususan katika eneo la ubunifu akisisitiza umuhimu wa kwenda na kasi ya mabadiliko hayo.
“Lengo ni kujenga mazingira bora ya biashara nchini, sambamba na kutambua nafasi ya ubunifu katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi, tusiachwe nyuma, twende na kasi ambayo dunia inakwenda Itifaki zinazopendekezwa kuridhiwa zinalenga kuimarisha mfumo wa ulinzi wa ubunifu na kuwapa wabunifu fursa ya kushindana katika soko la kimataifa” alisema Bi. Mhando.
Itifaki nne ambazo zimejadiliwa katika Kikao hicho ni pamoja na Itifaki ya Banjul ya Alama; Itifaki ya Madrid ya Usajili wa Alama Kimataifa, Itifaki ya Arusha ya Ulinzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea, na Itifaki ya Kampala ya Usajili wa Hiyari wa Hakimiliki na Hakishiriki.
