Habari
BRELA YAIBUKA KINARA WA TAASISI ZA UWEZESHAJI BIASHARA NA UWEKEZAJI
BRELA YAIBUKA KINARA WA TAASISI ZA UWEZESHAJI BIASHARA NA UWEKEZAJI
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeibuka kinara wa kati ya taasisi zinazowezesha Biashara na Uwekezaji zilizoshiriki kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam na kupewa tuzo ya mshindi wa kwanza.
Katika maonesho hayo BRELA imeendelea kutetea nafasi yake ya mshindi wa kwanza ikifuatiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Maonesho hayo yamefungwa rasmi leo Julai 13, 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) mara baada ya zoezi la ugawaji tuzo na vyeti kwa Washindi bora na Wadhamini hayo.
Ikumbukwe kuwa BRELA ilikabidhiwa tuzo hiyo Julai 7, 2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo (Mb) wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa maonesho hayo iliyoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Seka Kasera, Meneja wa Sehemu ya Alama za Biashara na Huduma alieleza kuwa ushindi huo umetokana dhamira ya Taasisi ya kuhakikisha inaweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji.
“Katika Maonesho ya 45, BRELA ilishika nafasi ya tatu katika kundi hili. Tangu wakati huo, tulidhamiria kushika nafasi ya kwanza kwa kuhakikisha kila mteja anayefika kwetu anapata huduma bora na za haraka.
Katika Maonesho ya 46, tulipanda hadi nafasi ya pili, na tangu Maonesho ya 47, tumeshinda nafasi ya kwanza na kuendelea kutetea nafasi hiyo. Hatuboreshi huduma zetu kwenye maonesho tu, bali hata baada yake, ili kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara na wawekezaji,” alisema Bw. Kasera.
Katika kipindi chote cha maonesho, BRELA ilitoa huduma za papo kwa papo zinazopatikana kwa njia ya mtandao, jambo lililowavutia wadau mbalimbali. Mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao ORS umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza urasimu, kuongeza ufanisi na kuwezesha wananchi wengi zaidi kurasimisha biashara kwa urahisi na haraka.