Habari
BRELA YAIPA HAMASA KLABU YA IP KIEMBE SAMAKI SEKONDARI
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kushirikiana na Shirika la Hakimiliki Tanzania (COSOTA)imeendelea kuhamasisha ubunifu miongoni mwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini, kupitia ziara za kutembelea Klabu za Miliki Ubunifu.
Akizungumza katika ziara iliyofanyika Sekondari ya Kiembe Samaki, Zanzibar tarehe 06 - 07 Novemba 2026, Afisa Usajili kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu BRELA Bw. Benedickson Wilson amesema lengo la ziara hiyo ni kutathmini bunifu mbalimbali za wanafunzi wa Klabu ya Miliki Ubunifu shuleni hapo, ambazo zitawasilishwa kwenye Mashindano ya Miliki Ubunifu kwa shule za sekondari yanayoratibiwa na Shirika la Miliki Ubunifu la Kikanda la Afrika (ARIPO).
Bw. Benedickson Wilson, alibainisha pia Klabu za Miliki Ubunifu Shuleni ni jukwaa muhimu la kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda kazi zao za ubunifu, kutambua thamani ya mawazo yao, na kutumia mifumo rasmi ya usajili wa Alama za Biashara, Hataza na Haki Miliki.
“Tunataka kuona vijana wakikua wanakuwa wabunifu wenye uelewa wa haki zao, elimu hii itawasaidia si tu kubuni bali pia kulinda na kunufaika na kazi zao kwa siku za mbele.” alisisitiza Bw. Willison.
Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha shule tano kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambazo ni Makongo Sekondari, St. Joseph, Ufundi Tanga, Sikirari ya Kilimanjaro na Kiembe Samaki ya Zanzibar.
Kupitia mashindano haya, BRELA inaendelea kutoa msukumo kwa shule nyingine nchini kuanzisha Klabu za Miliki Ubunifu ili kukuza kizazi cha wabunifu wenye uelewa wa kisheria kuhusu miliki zao na mchango wao katika maendeleo ya taifa.
