Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YAPONGEZWA KWA KUTEKELEZA “BLUE PRINT”


BRELA YAPONGEZWA KWA KUTEKELEZA “BLUE PRINT”

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Hanafi Msabaha ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa kutekeleza Mpango wa Utekelezaji wa Mkakati wa “Blueprint”
(MKUMBI) yenye nia ya kuboresha Mazingira ya Biashara nchini.

Mhe. Msabaha amebainisha hayo leo Mei 10, 2023 wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Maafisa Biashara kutoka katika Mikoa 10 ya Tanzania Bara kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu, hasa kwa kuzingatia kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini, ili kuendana na azma ya kufanya mageuzi ya kiuchumi.

“Nawapongeza sana BRELA kwa kuandaa na kuratibu mafunzo haya muhimu kwa Maafisa Biashara, ikiwa pia ni njia mojawapo ya utekelezaji wa “Blueprint” yenye nia ya kuboresha mazingira ya biashara nchini. Juhudi hizi ni nzuri na zitaleta matokeo chanya katika ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini” amesema Mhe. Msabaha.

Aidha amebainisha matarajio yake kuhusu mafunzo yanayotolewa kuwa yatasaidia Maafisa Biashara kubadili fikra na mitazamo na kuwa watoa huduma na msaada kwa wafanyabiashara.

Awali akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, Mkuu wa Sehemu ya Leseni za Biashara, Bw. Tawi Kilumile ameeleza kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 10 hadi 12, 2023.

Lengo kuu ni kuwajengea uelewa na uwezo Maafisa Biashara wa kusimamia Sheria ya Leseni za Biashara (Sura 208) na Sheria ya Taifa ya Usajili wa Leseni za Viwanda (Sura 46), kwa ufasaha wanapotekeleza majukumu yao na hatimaye kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.

Ametoa rai kwa Maafisa kutokujikita katika ukusanyaji mapato kama ilivyokuwa hapo awali, bali kuwa marafiki na washauri wa wafanyabiashara kwani kukua kwa biashara ndiyo kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Maafisa Biashara wanaoshiriki katika mafunzo hayo ni kutoka Mikoa ya Lindi, Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Pwani, Morogoro Dar es Salaam na Mtwara.