Habari
BRELA YASHAURIWA KUONGEZA WIGO WA ELIMU KWA WADAU WAKE MKOA WA MBEYA
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, ameishauri Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuendelea kutoa elimu ya urasimishaji wa biashara ili kuwafikia wananchi na wajasiriamali wengi zaidi hasa maeneo ya vijijini.
Mhe. Malisa alitoa ushauri huo tarehe 26 Mei, 2026 alipotembelea banda la BRELA kwenye Maonyesho ya Biashara ya Mbeya City Expo 2026 kuona jinsi huduma mbalimbali zinazotolewa kwa njia ya mtandao ambapo alipata fursa ya kukabidhi cheti cha usajili Jina la Biashara kwa mteja aliyepata huduma ya papo kwa papo.
"BRELA mnatakiwa muendelee kujitangaze zaidi kwa wananchi ili wajue huduma mnazozitoa na umuhimu wake, shukeni chini hadi ngazi ya wilaya na vijiji mtoe elimu hii ya urasimishaji. Wananchi hasa wafanyabiashara wa pembezoni bado wanahitaji kufahamu zaidi taratibu za kuwa rasmi kwenye biashara,” alisisitiza RC Malisa.
Kwa upande wake, Afisa Leseni Mwandamizi kutoka BRELA Bw. Koyan Aboubakar alisema kuwa Wakala imejipanga na imedhamiria kuwahudumia wananchi wote wanaotembelea banda huku akisisitiza kuwa urasimishaji unawasaidia wafanyabiashara kufungua milango ya mafanikio kwenye biashara zao.
BRELA inaendelea kutoa huduma za papo kwa papo na elimu ya usajili wa majina ya biashara, makampuni na leseni katika banda lao lililopo katika viwanja vya uhindini kwenye maonyesho hayo yanayotarajiwa kuhitimishwa tarehe 30 Mei, 2026.
