Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI KITAIFA MKOANI SINGIDA


BRELA YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI KITAIFA MKOANI SINGIDA

Wakala wa Usajilii wa Biashara na Leseni (BRELA) leo tarehe 1 Mei, 2025 imejumuika na wafanyakazi wengine kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi nchini katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, (MEI MOSI).

Maadhimisho ya Mei Mosi Kitaifa  yamefanyika mkoani Singida na kuhudhuriwa na watumishi wa sekta mbalimbali za umma na binafsi kutoka maeneo yote nchini ili kutambua mchango wa wafanyakazi katika kuletea taifa maendeleo.

Katika hotuba yake Mgeni Rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amevitaka vyama vya wafanyakazi kuendelea kutetea maslahi ya wafanyakazi huku akiwasihi watumishi wa taasisi za umma na binafsi kushikamana katika mapambano ya vita ya kiuchumi ili kulinusuru taifa.

Aidha, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza ongezeko la asilimia 35.1% la mishahara kwa kima cha chini kwa watumishi wa umma na ameahidi kuendelea kuboresha zaidi maslahi ya watumishi ili kuendeleza ustawi wao.

Rais Dkt. Samia amesema maamuzi ya Serikali kupandisha mishahara yametokana na kasi ya ukuaji wa uchumi kupanda hadi kufikia 5.5% kwa mwaka, hali iliyochangiwa na wafanyakazi kujituma na kufanya kazi kwa bidii.

"Tutaendelea kuboresha mazingira ya wafanyakazi ikiwemo maslahi ya wafanyakazi kadiri hali itakavyoruhusu, kujenga nchi yetu ni jukumu letu sote, hivyo hatuna budi kuimarisha umoja na mshikamano wetu. Historia ya vyama vya wafanyakazi ni vyama vilivyoleta vuguvugu la uhuru wetu, tusitumike kusaliti uhuru wetu," amesisitiza Rais Dkt. Samia

Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu yamefanyika mkoani Singida na  yamekuja na kauli mbiu isemavyo “Uchaguzi Mkuu wa 2025 utuletee Viongozi wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote tushiriki.”