Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YATIMIZA AHADI YA KUWALETA WATOTO YATIMA KITUO CHA TUYATA MJI WA SERIKALI MTUMBA


BRELA YATIMIZA AHADI YA KUWALETA WATOTO YATIMA KITUO CHA TUYATA MJI WA SERIKALI MTUMBA

WATOTO Yatima na wenye Ulemavu 100 kutoka Kituo cha Kulelea Yatima cha Tulee Yatima Tanzania (TUYATA) kutoka Dar es Salaam wametembelea Mji wa Serikali Mtumba Dodoma huku wakiishukuru Wakala wa Usajili wa  Biashara na Leseni ( BRELA) kwa kudhamini ziara ya mafunzo kwa kutumia reli ya kisasa (SGR).

Akizungumza kwa niaba ya BRELA ya Afisa Mtendaji Mkuu Bw Godfrey Nyaisa, Afisa Habari Mkuu, BRELA Bi. Joyce Mgaya amesema  ziara hiyo inaonesha dhamira ya BRELA katika kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.

“Mtendaji Mkuu wetu aliona ni jambo jema kuwapa watoto hawa fursa ya kutembelea makao makuu ya nchi na kujionea miradi ya maendeleo inayotekelezwa,” amesema Bi Mgaya.

Hata hivyo ameongeza kuwa kwa wengi wao,ni mara ya kwanza kupanda treni ya SGR na kufika Dodoma, na kwamba ziara hiyo ni sehemu ya mikakati ya BRELA kusaidia jamii kupitia programu mbalimbali za kuwafikia wananchi.

Aidha Bi.Mgaya  ametoa wito kwa Taasisi zingine ziendelee kuwakimbilia watu wenye mahitaji Kwa kuhakikisha wanawasaidia mahitaji mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi na Mwanzilishi wa kituo cha TUYATA, Bi Fauzia Jabir amesema kuwa wanaishukuru BRELA kwa safari hiyo kwani watoto wengi wamefurahi na katika maisha yao hawajawahi kupanda treni.

“Watoto wamefurahi mno, jambo hili halijawahi kutokea. BRELA imefanya jambo kubwa  kwa kusimama na watoto hawa wahitaji. Wamehamasika kusoma zaidi baada ya kuona uzuri na fursa zilizopo nchini,” amesema Bi Jabir.

Hata hivyo, ameeleza kuwa licha ya mafanikio ya kielimu waliyonayo, kituo hicho kinakabiliwa na changamoto kubwa ya makazi kwa watoto yatima, na hivyo kuomba msaada wa ujenzi wa nyumba za makazi kwa watoto na wajane.

Mmoja wa walionufaika na kituo hicho, Bi Ayman Jaffar Abubakar ambaye pia ni msemaji wa TUYATA, amesema kulea watoto kutoka mazingira mbalimbali si kazi rahisi lakini kwa neema ya Mungu, wanajitahidi kutoa malezi bora na kuwaelekeza katika njia sahihi.

“Watoto wengi wanaishi kwa walezi, hivyo ni changamoto kuwafuatilia kikamilifu. Tunaishukuru BRELA kwa kutuunga mkono na tunaomba waendelee kuwa nasi hadi tufikie malengo yetu,” amesema