Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

BRELA YATOA MAFUNZO YA MILIKI UBUNIFU KWA UONGOZI WA CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA CBE


Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku nne yaliyoanza tarehe 03 Februari, 2026, Afisa Sheria kutoka BRELA Bw. George Msaki alisema kutolewa kwa mafunzo haya kutaleta chachu ya usimamizi wa masuala ya Miliki Ubunifu pamoja na Urasimishaji wa Biashara nchini.

Aidha, katika mafunzo hayo BRELA kupitia Kurugenzi ya Miliki Ubunifu, imeendelea kuhimiza vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini kuanzisha klabu na madawati ya Miliki Ubunifu yatakayosaidia kukabiliana na changamoto ya uelewa wa masuala hayo miongoni mwa wakufunzi, watafiti na wanafunzi hususan katika maeneo ya Alama za Biashara, na Hataza.

Awali akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitalaamu Chuoni hapo Profesa Robert Mashenene alisema kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa watumishi kutokana na mabadiliko ya mwelekeo wa kiuchumi, ikilinganishwa na enzi za ujamaa, ambapo sasa watumishi wanahimizwa kuwa wabunifu na wajasiriamali.

Profesa Mashenene pia alieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia watumishi na wanafunzi kuona fursa mbalimbali za kibiashara zitakazowawezesha kuchangia katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na kuisaidia Serikali kukuza uchumi. Aliwasihi watumishi wenye taaluma mbalimbali kuanzisha na kurasimisha biashara.

“Na sisi watumishi tunayo fursa kubwa ya kushirikiana na Serikali kuweza kuongeza ajira kwa vijana. Mimi na wewe tukisajili majina ya biashara au makampuni na kuajiri vijana wasio na ajira, tutakuwa tumechangia moja kwa moja katika kupunguza tatizo hilo,” alisema Profesa Mashenene.