Habari
BRELA YATOA MSAADA KWA WATOTO WENYE UHITAJI
Akikabidhi msaada huo kwa watoto hao, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa BRELA Prof. Neema Mori amesema kuwa, “Wazo la mwaka huu ni ‘toa ili upokee’ hivyo nasi leo hii tumeshiriki kwa kutoa vitu mbalimbali ambavyo ni mahitaji yao ya kimwili na ya shule ili waendelee kwenda kuyatumia nyumbani na shuleni wakiwa kama watoto wetu,” alisema Prof. Mori.
Aidha, Prof. Mori ameongeza kuwa, katika kusherekea Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, BRELA imefanya kitu cha tofauti kwa kutoa muda kushiriki na wanawake wengine kusherekea, kupata elimu ya kukuza uchumi na kutenda matendo ya huruma ya kutoa kwa watoto wenye uhitaji.
Akirejea dira ya mwaka 2050, inayoanza rasmi kutekelezwa Julai mwaka huu, Prof. Mori alisema kuwa, BRELA imekuwa ikitembea na wazo la kuwa na ujumuishi katika kuwezesha kufikia ufanisi katika dira ya 2050, tunafahamu nguzo ya pili ya dira yetu inaangalia kujenga uwezo wa watanzania kwenye maeneo tofauti yakiwemo Ujasiriamali, Biashara, Vijana, Wanawake sambamba na kuwa na uwezo wa kuleta maendeleo katika jamii.
“BRELA tumejikita kutekeleza dira hiyo kwa kuchangia kwa sababu tunaamini kwamba BRELA ni kiungo muhimu katika kuchangia ukuzaji na ukuaji wa sekta binafsi nchini, hivyo tuko mstari wa mbele kuwezesha na kuhakikisha sekta binasi inakua kwa kuwawezesha wafanyabiashara sio tu kurasimisha biashara zao lakini pia kuhakikisha biashara zao zinakuwa bora zaidi.’’
Naye mlezi wa kituo hicho, Bw. Hamisi Suleiman, aliishukuru BRELA kwa msaada huo ambao umetolewa kwao na kusema kuwa ni kitu kikubwa ambao utawawezesha watoto hao kujikimu na kuziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo.
