Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YAWAHAMASISHA WAFANYABIASHARA ARUSHA KURASIMISHA BIASHARA ZAO


BRELA YAWAHAMASISHA WAFANYABIASHARA ARUSHA KURASIMISHA BIASHARA ZAO
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa wito kwa wafanyabiashara ambao bado hawajarasimisha biashara zao kufanya hivyo ili kuepuka changamoto mbalimbali za kibiashara.

Wito huo umetolewa leo tarehe 13 Desemba, 2023 na Afisa Sheria kutoka BRELA Bw. Edward Magayane, kwenye banda la BRELA nje ya ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC), jijini Arusha, linakofanyika Kongamano la 14 la mwaka la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi.

Aidha Bw. Magayane amesema katika kipindi cha kongamano, Maafisa wa BRELA wanatoa mwongozo kwa wadau wanaotembelea banda hilo juu ya mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS).
Bw. Magayane ameongeza kuwa mfanyabiashara anaporasimisha biashara yake, humuwezesha kupata fursa mbalimbali ikiwemo mikopo kutoka taasisi za kifedha, kupata zabuni zinazotangazwa serikalini na nyinginezo.
"Tunatoa ushauri na elimu kwa wadau wanaotembelea banda letu na wanaotaka kusajili kampuni na huduma nyingine wafike kwenye banda letu tutawapatia usaidizi," amesema Bw. Magayane. Kongamano hilo lililoanza tarehe 12 Desemba litahitimishwa tarehe 14 Desemba, 2023.