Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YAWAJENGEA UWEZO WADAU KUHUSU KANUNI ZA WAMILIKI MANUFAA WA KAMPUNI


 

BRELA YAWAJENGEA UWEZO WADAU KUHUSU KANUNI ZA WAMILIKI MANUFAA WA KAMPUNI
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imekutana na Vyombo vya Uchunguzi ili kuwajengea uwezo kuhusu dhana ya Kanuni za Wamiliki Manufaa wa Kampuni zinazomilikiwa na Wabia kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku kwakuwa ni watumiaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa.

Akifungua warsha ya siku moja katika ukumbi wa Ngorongoro Jijini Arusha, leo tarehe 8 Machi, 2023 kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Makampuni na Majina ya Biashara, Bw. Isidory Nkindi, amesema warsha hiyo italeta matokeo chanya katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, ushirikiano na utendaji wa vyombo vya uchunguzi, ili kuhakikisha BRELA inatoa huduma bora kwao na Umma kwa ujumla.

“Kampuni zina umuhimu mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi. Hata hivyo, uzoefu umeonesha kwamba baadhi ya kampuni zinatumika vibaya katika kufanya vitendo vya kihalifu visivyokubalika kwenye jamii, ikiwa ni pamoja na utakatishaji wa fedha haramu, kufadhili vitendo vya ugaidi, vitendo vya rushwa na hata ukwepaji wa kodi”, amefafanua Bw. Nkindi.

Pia amesema kupitia majadiliano haya, BRELA inategemea kukusanya maoni na ushauri kwa ajili ya maboresho zaidi ya utekelezaji wa Kanuni za Wamiliki Manufaa ili kuboresha utendaji kazi wa kila siku pamoja na kuhakikisha kuwa Vyombo vyote vya Uchunguzi
vinapata taarifa zenye uhakika na kwa wakati.

Kwa upande wake Mkaguzi kutoka Idara ya Uhamiaji, Bi. Beatrice Ngwijo, amesema warsha imekuwa ya manufaa hasa katika utekelezaji wa utoaji wa vibali vya Ukaazi kwakuwa watapata taarifa za kina kuhusu waombaji hao hasa wanapokuja kuwekeza nchini.

Akihitimisha warsha hiyo Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Bi. Eliainenyi Njiro, ameeleza kuwa mafunzo haya yatasaidia kuratibu upelelezi kwa weledi zaidi kwakuwa ni dhahiri kwamba kuna Kampuni zimesajiliwa BRELA lakini zinatumika katika kutenda uhalifu, hivyo dhana ya Wamiliki Manufaa itasaidia ofisi ya Taifa ya Mashtaka kupata taarifa sio tu za wamiliki wanaooneka kwenye katiba ya kampuni bali pia taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni.