Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YAWAPA ELIMU WAFANYABIASHA MKOA WA KILIMANJARO


BRELA YAWAPA ELIMU WAFANYABIASHA MKOA WA KILIMANJARO

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetembelea Mkoa wa Kilimanjaro kwa lengo la kutoa elimu ya huduma zinazotolewa na wakala pamoja na namna ya kutumia mifumo ya kielektroniki (BRELA Online Registration System and Beneficial Ownership Portal) kwa Kampuni.

Ziara hiyo kwa Kampuni, walielimishwa namna ya kuwasilisha taarifa mbalimbali kama vile Taarifa za Mwaka za Kampuni (Annual Return), pamoja na Taarifa za Wamiliki Manufaa (Beneficial Ownership Information), sambamba na huduma nyingine zinazotolewa na Msajili.

Akizungumza katika moja ya kaguzi hizo, afisa Sheria Mwandamizi kutoka BRELA, Bi. Anneth Enos Mfinanga, alisema kuwa lengo kuu la ukaguzi huo ni kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu wajibu wao baada ya usajili wa kampuni, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa za mwaka na taarifa za wamiliki manufaa, kama inavyotakiwa kisheria.
Aidha, alikumbusha kuhusu notisi ya Msajili, inayotangaza kusitisha huduma mbalimbali kwa wamiliki wa kampuni ambazo hazitakuwa zimewasilisha taarifa za wamiliki manufaa ifikapo tarehe 15 Aprili 2025.

Katika zoezi hilo, wafanyabiashara pia walielimishwa juu ya umuhimu wa kuhuisha taarifa zao kupitia mfumo wa kielektroniki wa BRELA (ORS), hasa kwa kampuni ambazo zimesajiliwa nje ya mfumo huo. Bi. Mfinanga alisisitiza kuwa huu ni wakati muafaka wa kutumia fursa ya msamaha wa 50% wa ada ya ucheleweshwaji wa taarifa za mwaka, msamaha ambao umetolewa na Waziri mwenye dhamana ya Viwanda na Biashara na utamalizika Mei 2025.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Yusuph Nzowa, aliipongeza BRELA kwa juhudi hizo na kuwasihi kuendeleza utoaji wa elimu hiyo mara kwa mara ili kuwawezesha wafanyabiashara kufahamu vyema majukumu ya Msajili na huduma zinazotolewa na wakala na hivyo kuwaongezea uwezo wa uendeshaji bora wa biashara zao.

Katika kipindi hicho, BRELA ilifanya ukaguzi elimishi kwa kampuni mbalimbali katika wilaya tatu za mkoa huo zikiwemo, Wilaya ya Siha kampuni 25, Wilaya ya Rombo: Kampuni 30, na Moshi Mjini: Kampuni 90. Hii inafanya jumla ya kampuni 145 zilizotembelewa na kupatiwa elimu juu ya huduma zinazotolewa na BRELA, pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumiaji wa mifumo hiyo na kusaidia namna bora ya kuitumia kwa usahihi.

Ziara hiyo elimishi ilianza tarehe 09 hadi 12 Aprili 2025 kwa ajili ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni kuhusu matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki ya BRELA pamoja na huduma mbali mbali zinazotolewa na BRELA,