Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA YAWAPATIA ELIMU WANAWAKE WAJASIRIAMALI


 

BRELA YAWAPATIA ELIMU WANAWAKE WAJASIRIAMALI

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa elimu kwa Umoja wa Wanawake Wajasiriamali kuhusu huduma zinazotolewa na Taasisi, kwa lengo la kuhamasisha urasimishaji wa biashara zao.

Elimu hiyo imetolewa leo tarehe 4 Januari, 2024 na Msajili Msaidizi kutoka BRELA Bi. Leticia Zavu katika ukumbi wa shule ya St. Anne Marie, Jijini Dar es Salaam.

Akiwasilisha mada katika semina hiyo Bi. Zavu ameelezea kuhusu huduma mbalimbali zinazo tolewa na BRELA ambazo ni pamoja na usajili wa Kampuni, usajili wa Majina ya Biashara, usajili wa Alama za Biashara na Huduma, utoaji wa Hataza, utoaji wa Leseni za Biashara kundi 'A' pamoja na utoaji wa Leseni za Viwanda.

Aidha Bi.Zavu ameeleza faida za kusajili Jina la Biashara kuwa ni pamoja na kulinda jina la biashara ili lisitumiwe na mtu mwingine, kutambulika na taasisi za kifedha , kupata mikopo katika taasisi za kifedha kama benki, biashara kutambulika kisheria, kuitangaza biashara kwa urahisi na kupanua wigo wa wateja.

Amewahimiza wajasiriamali hao kurasimisha biashara, kwani huduma zote hutolewa kwa njia ya mtandao, hivyo huduma hizo hupatikana mahali popote walipo.

BRELA imekuwa ikishiriki katika semina na mafunzo mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu ya urasimishaji wa biashara pamoja na kutoa usaidizi kwa wadau.

Semina hiyo ya siku moja iliyowashirikisha wanawake wajasiriamali wa kata ya Msigani, wilayani Ubungo, iliandaliwa na Umoja wa Wanawake Wajasiriamali (Tanzania Women Empowerment Network- TAWEN). ‎<This message was edited>