Habari
BRELA YAZITAKA KAMPUNI KUWASILISHA TAARIFA ZA MILIKI MANUFAA.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa wito kwa kampuni zote nchini kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa (Beneficial Ownership - BO) ili kuzingatia sheria ya Miliki Manufaa ya 2021.
Akizungumza katika kaguzi elimishi inayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 24 hadi Desemba 04, 2025, Afisa Usajili wa BRELA Bw. Englibert Lwabuhingi, amesema uwasilishaji wa taarifa hizo ni muhimu kwakuwa unasaidia kuzuia mianya ya uhalifu kama vile utakatishaji fedha, udanganyifu na kivuli cha kuficha taarifa nyeti.
“Dhana ya Umiliki Manufaa inatoa uwezo wa kumtambua kwa usahihi mtu anayenufaika au kudhibiti kampuni hata kama hayupo kwenye usajili wa kawaida, kutekeleza sheria hii ni njia ya kuzuia mianya ya uharibifu unaoweza kufanyika kupitia kampuni,” alisema Bw. Lwabuhingi.
Kampuni inayoshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa inajiweka katika mazingira hatarishi ya kisheria na kibiashara hasa katika kipindi ambacho dunia imeongeza masharti ya uwazi kwa taasisi za biashara.
“Kampuni zinahimizwa kuona uwasilishaji huu kama njia ya kuongeza hadhi, uaminifu na uwazi wa biashara zao na zinajenga mahusiano imara na wawekezaji pampja na wadau wengine wa kimataifa,” alisisitiza Bw. Lwabuhingi.
Kaguzi hizi, ni mwendelezo wa utekelezaji wa sheria ya dhana ya Miliki Manufaa ambapo kupitia zoezi hilo BRELA inatarajia kuongeza mwamko kwa wamiliki wa makampuni kutekeleza sheria hiyo na kuhakikisha taarifa za Miliki Manufaa zinawasilishwa kwa wakati na kwa usahihi.
