Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

CHUO KIKUU MZUMBE YAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA URASIMISHAJI BIASHARA KUTOKA BRELA


CHUO KIKUU MZUMBE YAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA URASIMISHAJI BIASHARA KUTOKA BRELA

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeitaka jumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe kuchangamkia fursa ya kurasimisha biashara zao ili ziweze kutambulika na  kulindwa kisheria. 

Hayo yamesemwa na Bi. Loy Mhando Mkurugenzi wa Miliki Bunifu kutoka BRELA wakati akiwasilisha mada kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara katika Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali 2024 yanayofanyika Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro.

 “Zipo faida nyingi zitokanazo na kurasimisha biashara zikiwemo, urahisi wa kufikiwa kwa huduma mbalimbali kwakuwa kutawezesha kupata takwimu sahihi za biashara na zitatambulika kisheria, mfanyabishara ataweza kuweka hesabu vizuri na kuweza kupata huduma za kibenki ikiwemo mikopo”. alisema Bi Mhando.   

Aidha Bi Mhando ameongeza kwa kusema kuwa, urasimishaji biashara utawezesha wafanyabiashara kulipa kodi ambayo itachangia katika kukuza uchumi wa taifa utakaowezesha ujenzi wa miundombinu ya kuwafikia wafanyabiashara sambamba na ujenzi wa masoko na uwekaji wa mazingira wezeshi ya biashara.   

Naye Iddi Mohamed mwanachuo wa mwaka wa pili katika chuo hicho ameeleza kuwa, amefurahishwa na elimu iliyotolewa na BRELA na kueleza kuwa, awali alikuwa na mawazo ya kuanzisha biashara yake lakini hakufahamu nini afanye, baada ya kupata elimu ya urasimishaji kutoka BRELA amepata uelewa kuwa ukisajili kampuni yako au biashara kwa ujumla unapata ulinzi wa kisheria na ikitokea changamoto yoyote unatambulika kirahisi.   

Katika Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali 2024, BRELA imeshiriki kwa kutoa mafunzo maalumu juu ya namna ya kurasimisha biashara wanazozifanya sambamba na kutoa huduma ya usajili wa papo kwa papo kwa wanafunzi na wafanyabiashara waliotembelea katika maadhimisho hayo.   

Tukio hilo linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 22 Machi, 2023 iliyobeba kaulimbiu isemayo “Kuzingatia Teknolojia Zinazoibukia na Njia Mpya za Kujifunza kwa Ajili ya Ukuaji Endelevu” inayolenga kuibua vipaji na mawazo bunifu ya wanafunzi wa chuo hicho na pia kutoa nafasi kwa wafanyakazi na wanafunzi kuonesha ubunifu walionao