Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

FURSA YA MILIKI UBUNIFU YAFIKA MAKONGO SEKONDARI


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa kushirikiana na Shirika la Hakimiliki Tanzania (COSOTA), inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhamasisha ubunifu miongoni mwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini kupitia ziara maalum za kutembelea Klabu za Miliki Ubunifu mashuleni.

Katika mwendelezo wa programu hii, tarehe 19 Novemba 2025, BRELA imetembelea Shule ya Sekondari Makongo TPDF, ambapo wanafunzi wanaounda Klabu ya Miliki Ubunifu (IP Club) walipata fursa ya kuwasilisha bunifu mbalimbali walizobuni kupitia klabu hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa kutoka BRELA, Bi. Juliet Kiwelu, alisisitiza umuhimu wa kubuni kazi za kipekee na zenye ubunifu wa hali ya juu, hususan bunifu zinazolenga kutatua changamoto katika jamii. Alieleza kuwa ubunifu wa aina hiyo unaweza kuwapa wanafunzi nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika Mashindano ya Miliki Ubunifu kwa Shule za Sekondari yanayoandaliwa na Shirika la Miliki Ubunifu la Kanda ya Afrika (ARIPO).

Ziara hiyo pia imelenga kutathmini bunifu zinazotekelezwa mashuleni, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano yajayo yatakayoshirikisha shule kutoka Tanzania Bara na Visiwani, zikiwemo Makongo Sekondari, St. Joseph, Ufundi Tanga, Sikirari Kilimanjaro, na Kiembe Samaki Sekondari kutoka Zanzibar.

BRELA inaendelea kusisitiza kuwa Klabu za Miliki Ubunifu ni jukwaa muhimu katika kuwajengea wanafunzi uelewa wa namna ya kulinda kazi zao za ubunifu, kutambua thamani ya mawazo yao, na kutumia mifumo rasmi ya usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Hataza na Hakimiliki.

Kupitia mashindano na ziara hizi, BRELA inalenga kukuza kizazi kipya cha wabunifu wenye uelewa wa kisheria kuhusu miliki zao na mchango wao katika maendeleo ya taifa.