Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

HUDUMA ZA PAPO KWA PAPO ZAMVUTIA WAZIRI JAFO KATIKA MAONESHO YA SABASABA


HUDUMA ZA PAPO KWA PAPO ZAMVUTIA WAZIRI JAFO KATIKA MAONESHO YA SABASABA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo, ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa maboresho ya haraka na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, hususan huduma za papo kwa papo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Saba Saba).

Akizungumza Julai 2, 2025, mara baada ya kutembelea banda la BRELA katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Mhe. Jafo alisema huduma zinazotolewa na wakala huyo ni kielelezo cha maendeleo ya kitaasisi na dira sahihi ya kuwahudumia wananchi kwa wakati.

“Nawapongeza sana BRELA kwa maboresho haya makubwa. Ni jambo la kuigwa kuona wananchi wakihudumiwa papo kwa papo bila usumbufu,” alisema Waziri Jafo, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi nyingine kuiga mfano huo.

Huduma zinazotolewa papo kwa papo na BRELA katika maonesho hayo ni pamoja na usajili wa Majina ya Biashara, Kampuni, Utoaji wa Alama za Biashara na Huduma pamoja na Utoaji wa Leseni za Biashara, huduma ambazo hapo awali zilihitaji muda mrefu kukamilika.

Waziri Jafo pia alihimiza BRELA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kusajili biashara na kufuata taratibu za kisheria, akisema kuwa hatua hiyo ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Maonesho ya mwaka huu yamekusanya taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, yakilenga kuhamasisha biashara, ubunifu, na uwekezaji nchini Tanzania.