Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA BRELA


KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA BRELA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeridhishwa na ufanisi wa utendaji kazi, ukuaji na mageuzi makubwa yaliyofanywa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa kuzingatia kuwa kigezo cha kwanza cha ufanyaji biashara Tanzania ni kupitia BRELA.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Deo Mwanyika (Mb), baada ya wajumbe wa Kamati hiyo kupata mafunzo juu ya majukumu ya BRELA leo tarehe 11 Februari, 2024 jijini Dodoma.

“Tumeyaona, tumeyasoma, tumeyasikia na kuyahoji zaidi tumeridhika sana na yale yanayofanyika ndani ya BRELA, mathalani ukitaka kuanzisha kampuni ndani ya siku mbili hadi tatu unapatiwa cheti chako ndani ya mfumo, vivyo hivyo kwa upande wa jina la biashara pia ni siku moja au masaa tu endapo utakuwa umekamilisha nyaraka zote zinazohitajika, baadhi ya wabunge wameshuhudia kuwa wameweza kusajili kwa muda mfupi, hivyo ni viashiria tosha kuwa Taasisi imejipanga na imeimarisha mifumo yake,” ameeleza Mhe. Mwanyika

Mhe. Mwanyika amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana jitihada anazozifanya za kuweka mazingira mazuri ya biashara ili Tanzania iweze kusonga mbele kwa kuwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na katika muktadha huo kupitia BRELA tumeona hatua kubwa iliyopiga, maana huo ndio uhai wa mazingira ya biashara.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb), akizungumza kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa Wizara inajukumu la kuhakikisha wananchi wanajua kazi zinazotekelezwa na Serikali kupitia taasisi zilizo chini ya Wizara, ambao ndio wadau wakubwa.

“Tunapokutana na nyie wawakilishi wao tunapata mrejesho kwa yale ambayo tunaweza kufanya vizuri kupitia BRELA, Taasisi ambayo ipo chini yetu, na pia kuona namna gani tunaenda kuchukua mawazo ambayo wananchi wangependa kuona Taasisi hii inafanya hasa katika usajili na utoaji wa leseni bila ukiritimba au urasimu usio na lazima, zaidi kutoa elimu kwa wananchi ukizingatia maeneo mengi yanahitaji wafanyabiashara wanaotambulika rasmi.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, amesema kuwa mbali na kuwaeleza majukumu ya Taasisi, BRELA inaendelea na kuboresha utendaji wake ikiwemo katika kufanya marekebisho ya Sheria ya Kampuni ambayo imepitwa na wakati, ili kwenda na wakati katika kuhudumia wafanyabiashara na kuhakikisha biashara zinakuwa.


BRELA imetoa mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati hiyo, ili kupata uelewa zaidi wa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa kutambua kuwa wabunge hao wana jukumu la kuisimamia Serikali ambalo ni la kikatiba na kuishauri. Katika kutekeleza hilo ni lazima wawe na ufahamu wa namna taasisi zinavyofanya kazi na kujua changamoto zao pamoja kuzipatia ufumbuzi.