Habari
KAMATI YA UKAGUZI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA YAISHAURI BRELA KUBORESHA KITENGO CHA UKAGUZI
Ushauri huo umetolewa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bi. Flora Kahabuka Masame wakati wa ziara ya Kamati ya Ukaguzi wa Ndani katika Ofisi za BRELA, iliyolenga kujifunza utekelezaji wa majukumu kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu zilizowekwa.
Bi. Masame alisema kadiri taasisi inavyoendelea kukua hakuna budi Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani nacho kikaimarishwa ili kiweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
“Tumeona utendaji mzuri wa BRELA, Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa amekitendea haki Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kwa kukiwezesha rasilimali watu na kuwajengea uwezo watumishi kupitia mafunzo na kuhakiksha kitengo kinakuwa na mkaguzi wa mifumo kusaidia kukagua maeneo ya mifumo.” alisema Bi. Masame.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Wizara Bw. Joseph Elias alieleza kuwa ziara hiyo imefanyika kufuatia maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, ambapo Kamati imekuwa ikitembelea taasisi zote zilizo chini ya Wizara ili kujifunza majukumu yanayotekelezwa na kubaini maeneo ya kuimarisha utendaji.
Aidha abainisha kuwa jukumu la Kamati ya Ukaguzi wa Ndani si tu kujifunza, bali pia kuhakikisha vitengo vya ukaguzi wa ndani vinaendeshwa kwa kuzingatia miongozo ya Serikali, sambamba na kufuatilia utekelezaji wa hoja za wakaguzi wa ndani, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na taasisi nyingine za ukaguzi.
Kamati hiyo ilibainisha kuwa eneo la Ukaguzi wa Mifumo ya TEHAMA (IT Audit) limekuwa changamoto katika taasisi nyingi, lakini BRELA imeonyesha jitihada za kuhakikisha mkaguzi wa TEHAMA anapatikana, hata kwa kushirikiana na taasisi nyingine, jambo linalosaidia kuhakikisha mifumo ya kidijitali inakaguliwa na kuendeshwa kwa ufanisi.
