Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

KUELEKEA SIKU YA MILIKI UBUNIFU DUNIANI BRELA NA COSOTA YAINOA TaSUBa


KUELEKEA SIKU YA MILIKI UBUNIFU DUNIANI BRELA NA COSOTA YAINOA TaSUBa

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inaendelea kutoa mafunzo kuhusu Miliki Ubunifu kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani ambapo leo tarehe 2 Mei, 2024 wametoa mafunzo katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) iliyopo Bagamoyo katika mkoa wa Pwani.

Katika mafunzo hayo Wanafunzi wameelekezwa kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA, upande wa Alama za Biashara na Huduma, Hataza pamoja na elimu ya Hakimiliki.

Awali akielezea huduma zinazotolewa na BRELA kwa Wanafunzi wa Taasisi TaSUBa, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Hataza Bi. Neema Kitala, amewataka wanafunzi hao wasisite kurasimisha biashara zao ili kuongeza wigo wa kutambulika na mamlaka mbalimbali na pia kuwawezesha kukopesheka katika Taasisi za kifedha.

Aidha, Meneja Idara ya Kumbukumbu na Usajili, Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Bw. Philemon Kilaka, ametoa msisitizo kwa wanafunzi wa Taasisi hiyo kusajili kazi zao za ubunifu katika Ofisi za Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili waweze kunufaika na kazi zao.

“Urasimishaji una faida nyingi ikiwemo usimamizi wa kusimamia kazi zenu kwa ufanisi, kulindwa na sheria ya Hakimiliki na kupata fursa za biashara zaidi kwa kuwa mtakua mnatambulika. Vilevile, mtaweza kuongeza kipato binafsi na cha Taifa kwa ujumla, pamoja na kupanua soko la kazi zenu”, amesisitiza Bw. Kilaka.

Naye Bw. Calvin Rwambogo, Afisa Sheria kutoka BRELA amewahimiza Wanafunzi hao kuchukua hatua ya kuanza mchakato wa kusajili Bunifu zao BRELA, kabla ya kupeleka katika jamii ili kuepuka kuibiwa Bunifu husika.

Mafunzo ya Miliki Ubunifu Mjini Bagamoyo yamefanyika ndani ya siku moja ambapo pamoja Taasisi hiyo, BRELA imefikisha elimu ya Miliki Bunifu katika Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Taasisi ya Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Innovation Hub ya Taasisi ya Afya ya Ifakara na Kiatamizi (Incubator) cha Ubunifu kijulikanacho kama TAOTIC na inaendelea kutoa elimu hii.