Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

TANZANIA INAHITAJI ALAMA YA BIASHARA YA KIPEKEE KUTAMBULISHA BIDHAA ZA KILIMO NJE YA NCHI


TANZANIA INAHITAJI ALAMA YA BIASHARA YA KIPEKEE KUTAMBULISHA
BIDHAA ZA KILIMO NJE YA NCHI- BASHE
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe(Mb) amesema imefika wakati sasa kwa Taasisi
zinazohusika na masuala ya Miliki Ubunifu kuja na mapendekezo yatakayowezesha
Tanzania kuwa na alama ya biashara ya kipekee itakayotambulisha bidhaa za
Tanzania duniani kote.
Waziri Bashe ametoa rai hiyo tarehe 02 Novemba, 2022 jijini Dodoma alipotembelewa
ofisini kwake na ujumbe kutoka Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO)
ambalo makao makuu yake yako Harare- Zimbabwe, ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu
wa Shrikika hilo Bw. Bemanya Twebaze, aliyeambatana na Mwenyeji wake Afisa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey
Nyaisa.
Mhe. Bashe amesema Tanzania ikiwa na alama yake ya biashara ya kipekee mfano
kwa bidhaa zake zote za kilimo zinazouzwa nje ya nchi itawezesha kutambulika duniani
kote na thamani ya bidhaa hizo kuongezeka tofauti na ilivyo sasa ambapo bidhaa nyingi
zinauzwa nje ya nchi lakini hazitambuliki kama bidhaa za Tanzania kama nchi. Pia
kutumika kwa Alama ya Tanzania kutazitangaza bidhaa za kilimo kutoka Tanzania. Hii
itasaidia kujua mnyororo wa thamani wa bidhaa zote za kilimo.
“Ukiangalia bidhaa ya Champagne ni mvinyo unajulikana duniani kote kutokana jina la
mahali bidhaa hiyo ilikozalishwa kwa mara ya kwanza nchini Ufaransa, Ifike wakati sasa
bidhaa za Tanzania zijulikane kwa alama ya kipekee duniani kote”, amesisitiza Mhe.
Bashe.
Akizungumzia Ufadhili wa wanafunzi watano kila mwaka wanaosomea Shahada ya
Uzamili ya Masuala ya Miliki Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya
ufadhili wa BRELA, wakati ARIPO ikitoa utaalam wa kiufundi na ufadhili, ameshauri pia
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia
(COSTEC) pia zijumuishwe kwenye mpango huo kwani vumbuzi nyingi zinafanyika
katika taasisi hizo hivyo ni vyema zikawezeshwa zaidi.
Mhe. Bashe amesema katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na ARIPO za
kuendeleza Miliki Ubunifu kwa nchi wananchama wa ARIPO wizara yake itaridhia Itifaki
ya Arusha inayohusu ubunifu wa aina mpya ya mbegu za mimea iliyosainiwa Arusha
mwaka 2015 na kuelekeza viongozi wa Wizara ya Kilimo kuanza mchakato wa
kuridhiwa kwa Itifaki ya Arusha, kwani haileti picha nzuri kwa kutoridhia Itifaki
iliyosainiwa mwaka 2015 Mkoani Arusha.
Awali akimtambulisha Bw, Twebaze, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw, Nyaisa
amesema BRELA ikiwa ni miongoni mwa wanachama wa ARIPO imekuwa ikinufaika na

mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Shirika hilo ya kuwajengea uwezo watumishi
wa BRELA.
Bw. Nyaisa amesema BRELA inatambua umuhimu wa Miliki Ubunifu kwa Tanzania
ndiyo maana imekuwa mstari wa mbele kutoa ufadhali wa masomo kwa Watanzania ili
wawe chachu katika kuhakikisha kuwa wabunifu wananufaika na bunifu zao na
kulindwa kisheria.
Kwa upande wake Bw, Twebaze ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano
ambao ARIPO inaupata kupitia BRELA kwani ujumbe huu ukiwa nchini Tanzania
umekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya Umma zinazojihusisha na masuala ya
Ubunifu wa aina mpya ya mbegu za mimea chini ya Itifaki ya Arusha ambayo inasubiri
kuridhiwa.
Ameeleza pia baada ya kufanya ziara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
kuzungumza na uongozi wa chuo hicho ameridhishwa na mashirikiano yaliyopo kati ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na BRELA katika kufanikisha ufadhili wa masomo ya
Shahada ya Uzamili kwa wanafunzi ambao wanatoka nchi wanachama wa ARIPO
ikiwemo Tanzania.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uwekezaj, Viwanda na Biashara Mhe, Exaud
Kigahe (Mb) alipokutana na ujumbe huo wa ARIPO katika ofisi za BRELA jijini Dodoma,
ameahidi wizara yake kufuatilia kwa karibu ili Itifaki ya Arusha iridhiwe mapema na
kuanza kutumika ambayo itawezesha upatikanaji wa mbegu na uzalishaji wa chakula
cha kutosha kutokana na ubunifu wa aina mpya ya mbegu za mimea.
“Itifaki hii ni muhimu na itaridhiwa mapema iwezekanavyo kwani nchi inahitaji
kujitosheleza kwa chakula hivyo ni vyema bunifu hizi zikalindwa ikiwa ni pamoja na
wahusika kunufaika”, amesisitiza Mhe, Kigahe.
Ujumbe wa ARIPO ambao umeondoka leo tarehe 3 Novemba, 2022 kurejea nchini
Zimbabwe umekuwepo nchini kwa siku nne na mbali ya kukutana na viongozi pamoja
na wadau, pia ulipata fursa ya kutembelea mji wa Serikali wa Magufuli uliopo Mtumba
jijini Dodoma, pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa
ambapo Bw. Twebaze amepongeza maendeleo yanayofanywa na Serikali chini ya
uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungazo wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mwisho.