Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

UADILIFU NA MAADILI VYASISITIZWA KWA WATUMISHI WA BRELA


Hayo yamejiri wakati wa mafunzo maalum kuhusu Mkakati wa Taifa wa kuimarisha Maadili na Uadilifu kwa Watumishi wa Umma, yaliyoandaliwa na BRELA na kufanyika katika Ukumbi wa Golden Jubilee, PSSSF jijini Dar es Salaam.

Akifungua mafunzo hayo, Afisa Utawala Mwandamizi wa BRELA, Bw. Hamad Namohe, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuwajengea watumishi uelewa na kuwakumbusha wajibu wao wa kutekeleza majukumu kwa kuzingatia maadili, sheria na taratibu za kazi.

Katika mada iliyowasilishwa na Afisa Mkuu kutoka Dawati la Uelimishaji TAKUKURU, Bi. Theopista Naluyaga, aliwataka watumishi kuzingatia uadilifu katika utendaji kazi na kuepuka vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufuata sheria na kanuni za kazi.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Fabian Pokela, aliwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili katika utumishi wa umma, akieleza kuwa uadilifu ni msingi muhimu wa kujenga taasisi imara na kuongeza imani ya wananchi kwa serikali.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za BRELA za kuimarisha utamaduni wa maadili, uwajibikaji na utendaji kazi wenye tija kwa watumishi wake, ili kuhakikisha taasisi inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya sekta ya biashara nchini.