Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

UJUMBE WA ARIPO WAKUTANA NA WADAU


UJUMBE WA ARIPO WAKUTANA NA WADAU

Ujumbe kutoka Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO), unafanya ziara nchini kwa kukutana  na wadau wa sekta za umma zinazojihusisha na masuala ya ubunifu wa aina mpya za mbegu za mimea (protection of new varieties of plants) chini ya Itifaki ya Arusha ya Ulinzi wa Aina mpya za Mbegu.

Ujumbe huo ukiongozwa na Mkurugenzi mkuu wa ARIPO kutoka Makao makuu nchini Zimbabwe Bw. Bemanya Twebaze umepokelewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),   mwenyeji wa ujumbe huo, ambapo kwa kushirikiana na Wataalam hao,  umefanya semina kuhusu Itifaki ya Arusha ya Ulinzi wa Aina Mpya za mbegu iliyofanyika  Leo Novemba 1, 2022 Jijini Dar es salaam, ili kujadili kwa kina  kuhusu ulinzi wa aina mpya za mimea.

Akitoa neno la ufunguzi katika kikao hicho Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA   Bw. Godfrey Nyaisa amesema, Tanzania kama  mwanachama wa ARIPO, imechukua jukumu hili ili kutoa nafasi kwa wabunifu mbalimbali kupata ufahamu utakaowasaidia kuendelea kulinda haki zao kupitia ubunifu wa aina mpya za mbegu za mimea, ikizingatiwa  kwamba mbegu bora zaidi zinahitajika kwa wingi ili kuongeza uzalishaji na kuleta kuhakika wa chakula.

Bw. Nyaisa ameeleza zaidi kwamba  "BRELA kama taasisi inayohusika na masuala ya usajili na uhifadhi wa kumbukumbu za bunifu mbalimbali, kwa kuzingatia majadiliano kuhusu ulinzi wa aina mpya za mimea, imetenga fedha katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 ili  kuhakikisha wabunifu wanapewa elimu ikiwemo kuwatembelea katika maeneo ya ubunifu na hasa  katika vyuo mbalimbali vinavyotoa elimu na kufanya tafiti ili kulinda bunifu zao na kupata faida zitokanazo na ulinzi wa bunifu.

Aidha, BRELA itahakikisha kuwa elimu ya Miliki Ubunifu inawafikia wadau wote wanaohusika ikiwemo  ulinzi wa aina  mpya za mimea kwa kuandaa semina mbalimbali na mafunzo yenye tija, ili wabunifu wafahamu nini wanachotakiwa kusajili na manufaa ya kuongeza thamani ya bunifu zao",
Tangu Mwaka 2018 BRELA ilianzisha mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS), ambao umewezesha Usajili kuanzia hatua za maombi mpaka kukamilika  na pia mfumo umewezesha wadau kupata taarifa mbalimbali za Usajili wa bunifu.

Kwa upande wake Bw. Twebaze ameshukuru mapokezi mazuri   na ushirikiano walioupata kutoka BRELA  na kueleza kuwa hali hii itawezesha dhima kuu ya ARIPO ya kuwafikia  wadau ambao ndiyo wamiliki wa bunifu hizo na kupata manufaa zaidi.

Bw. Twebaze ameongeza kuwa ujumbe huo  umeshatembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kushuhudia bunifu mbalimbali ambazo zinatia matumaini kuwa uelewa wa masuala ya miliki ubunifu unaongezeka zaidi hivyo Shirika la ARIPO litaendelea  kutoa ushirikiano kwa BRELA ili wabunifu wengi zaidi waweze kulinda bunifu zao ikiwemo aina mpya za mbegu za mimea.

Aidha,  amewataka wadau waliofika katika semina hiyo  kuwa na mchango chanya kwani maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaenda sambamba na ubunifu, hivyo taasisi zinazohusika hazina budi kuungana na kutoa elimu ili wabunifu wengi waweze kulinda bunifu zao.

"Ikiwa kilimo kinazidi kukua kila siku,  ulinzi wa aina mpya za mbegu mimea umelenga kuongeza chachu katika ubunifu mpya wa mbegu  za mimea na kulinda bunifu hizo  na kutambulika katika maeneo mengine", amesisitiza Bw. Twebaze.