Habari
WANAFUNZI 2,000 WA CBE DAR ES SALAAM WANUFAIKA NA MAFUNZO YA MILIKI UBUNIFU KUTOKA BRELA
Mafunzo hayo ambayo yameendeshwa kwa siku nne chuoni hapo, yamelenga kuchochea ubunifu miongoni mwa vijana na kuwawezesha kulinda bunifu zao na kunufaika kupitia ulinzi huo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Sheria kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu BRELA, Bw. George Msaki aliwaeleza wanafunzi hao kusajili na kulinda Alama za Biashara (trademarks) ni njia ya kulinda ubunifu dhidi ya wizi wa mawazo na matumizi yasiyo halali, sambamba na kuongeza thamani na uaminifu wa bidhaa na huduma zao sokoni.
“Unaposajili Alama ya Biashara, Mali Bunifu yako au ukilinda vumbuzi wako, hii inakupa wewe mbunifu ulinzi wa kisheria kunufaika na ubunifu ambao tunasema ni zao la akili yako” alisema Bw. Msaki.
Aidha, Bw. Msaki alisema elimu hiyo inalenga zaidi kuhakikisha wanafunzi wanapata msaada wa kitaalamu ndani ya mazingira ya chuo na kuchochea ubunifu, ujasiriamali na matumizi sahihi ya Haki za Miliki Ubunifu miongoni mwa vijana.
Alisitiza uongozi wa Chuo kuanzisha Dawati la Miliki Ubunifu pamoja na Klabu ya Miliki Ubunifu itakayosaidia kutoa elimu, ushauri na msaada wa karibu kwa wanafunzi katika masuala ya ubunifu kama vile usajili wa Alama za Biashara na Vumbuzi mbalimbali.
Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara BRELA, Bi. Neema Nyadzi aliwasisitiza wanafunzi kuwa hawapaswi kuendesha biashara zisizo rasmi, akieleza kuwa elimu wanayoipata inapaswa kuwa chachu ya kuanzisha biashara zilizosajiliwa na zenye muundo bora wa uendeshaji.
Awali, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Robert Mashenene alisema elimu hiyo imekuja wakati muafaka kwa kuwa inalenga kuwaandaa wanafunzi kutumia maarifa wanayopata chuoni katika kuanzisha na kuendesha biashara halali zenye tija na zinazozingatia misingi ya kisheria.
