Habari
WANAFUNZI WA KLABU YA MILIKI UBUNIFU WATAKIWA KUWA MABALOZI WA ELIMU KWA WENGINE
Wito huo umetolewa tarehe 13 Januari, 2026 na Msajili Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu, BRELA, Bi. Neema Kitala wakati wa Mafunzo maalumu kwa viongozi wa Klabu ya Miliki Ubunifu kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya.
Kupitia Mafunzo hayo, wanafunzi wameelimishwa juu ya faida za Miliki Ubunifu na taratibu za usajili wa Alama za Biashara na Huduma, pamoja na Hataza ili waweze kuwahamasisha wenzao chuoni kujiunga na Klabu hiyo kwa wingi zaidi na kutumia fursa zilizopo.
Akizungumza baada ya Mafunzo, mwanafunzi Agnes Magesa amesema mafunzo hayo yamewasaidia kwa kiasi kikubwa kuelewa namna ya kulinda na kutetea bunifu zao wakiwa Chuoni na pindi watakapohitimu na kuingia katika mazingira halisi ya kazi na ubunifu.
“Tumejifunza vitu vingi ambavyo vitatusaidia sisi kama wanafunzi tutakapotoka chuoni, tumepata uelewa wa namna ya kuwasaidia wenzetu kulinda bunifu zao na kueneza maarifa haya kwa wale wasio na ujuzi wa Miliki Ubunifu,” amesema Magesa.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Mbeya ambaye pia ni Mlezi wa Klabu ya Miliki Ubunifu Chuoni hapo Dkt. Kennedy Makafu amesema, Chuo hicho kimejipanga kuhakikisha wanafunzi walionufaika na mafunzo hayo wanakuwa walimu wa wenzao, ili kuongeza idadi ya wanafunzi wenye uelewa wa Miliki Ubunifu kuelekea katika utekelezaji wa vitendo wa kulinda na kusajili bunifu mbalimbali miongoni mwa wanafunzi.
“Wenzetu BRELA wana uzoefu mkubwa wa masuala haya. Sisi Chuoni tumekuwa tukifundisha zaidi nadharia, lakini kupitia Mafunzo haya tumejifunza kwa vitendo namna Miliki Ubunifu inavyosajiliwa na nani wanaonufaika,” amesema Dkt. Makafu.
