Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

WAPENDEKEZA ELIMU YA MILIKI UBUNIFU IFUNDISHWE KUANZIA SHULE ZA MSINGI


 

WAPENDEKEZA ELIMU YA MILIKI UBUNIFU IFUNDISHWE KUANZIA SHULE ZA MSINGI

Washiriki wa mafunzo ya Miliki Ubunifu katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido wamependekeza kuwa ili idadi ya wavumbuzi Tanzania iongezeke, elimu ya Miliki Ubunifu itolewe kuanzia ngazi ya shule ya msingi Ili kuwaandaa wanafunzi kuwa wavumbuzi wakiwa bado wadogo.

Akichangia mada baada ya wasilisho kuhusu umuhimu wa kusajili vumbuzi mbalimbali lililotolewa na Afisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Benedickson Byamanyilwowa leo tarehe 30 Novemba, 2023 wilayani Longido, mfanyabiashara Bw. Elisante Mwasha amesema elimu ya Miliki Ubunifu ni muhimu kufundishwa kuanzia ngazi ya shule za msingi ili kuwajengea uelewa wa kutosha na hatimaye kuzalisha wavumbuzi wengi nchini na kuzisajili vumbuzi hizo BRELA .

"Elimu mliyotupatia leo ni nzuri sana lakini naona kama imechelewa na endepo ningekuwa na elimu hii muda mrefu, mbali na biashara ninazofanya ningeweza kuvumbua vitu mbalimbali na kunufaika na uvumbuzi wangu," alifafanua Bw. Mwasha.

Awali Bw. Byamanyilwowa aliwaeleza washiriki hao kuwa pamoja na kwamba BRELA imekuwa ikitoa elimu na kuhamasisha wadau kusajili vumbuzi zao bado idadi ya maombi hairidhishi.

Kutokana na hali hiyo BRELA imejikita katika kutoa elimu kuhusu Miliki Ubunifu katika vyuo vya kati na vyuo vikuu ili kukuza uelewa wa vijana kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu ambayo wakiizingatia itawanufaisha kwa kuwapatia ajira.

"Hakuna maisha bila hataza, vumbuzi inaongeza ajira, inamwezesha mvumbuzi kubaki katika ushindani ndani na nje ya nchi na zaidi inampa haki ya kipekee ya kumzuia mtu yoyote kutumia vumbuzi yake,"ameeleza Bw. Byamanyilwowa.

Akielezea kuhusu vigezo vya uvumbuzi kama ilivyoanishwa katika Sheria inayolinda uvumbuzi sura 217 amesema, Uvumbuzi ni ule unaotatua changamoto katika jamii kwa kutoa suluhisho la changamoto hiyo au tatizo hilo, mfano mvumbuzi aliyevumbua miwani alilenga kutatua changamoto ya mtu mwenye tatizo la uoni hafifu wa kuona karibu au mbali, hivyo basi mvumbuzi huyo akatatua changamoto hiyo kwa kuvumbua miwani yenye lenzi za kuona karibu na kuona mbali.

Kisheria uvumbuzi lazima uwe ni mpya, uvumbuzi huo ukisajiliwa unalindwa kwa miaka 20 na mvumbuzi anachopaswa kufanya ni kuhuisha vumbuzi yake kwa kulipa shilingi 4,000/= kwa mwaka wa kwanza na baada hapo atatakiwa kuhuisha kila mwaka kwa gharama ya shilingi 1000/= , huku ghaharama za awali za usajili na kupata cheti nikiwa ni shilingi 22,000/=.

Kwa upande wake Afisa Sheria wa BRELA Bw. Andrew Malesi akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kusajili logo amesema logo ni mali kama mali nyingine, hivyo endapo itasajiliwa inaweza kuuzwa au kutumiwa na mtu mwingine kwa makubaliano maalum na mmiliki wa logo husika.

Amewaeleza kuwa matumizi ya logo ni kwa wafanyabiashara wote kuanzia wadogo, wa kati na wakubwa hivyo ni muhimu wakabuni logo za biashara zao na kuzisajili ili waweze kijitofautisha sokoni, kujitangaza na hata kutumiwa na mtu mwingine kwa makubaliano maalum na mmiliki wa logo husika.

BRELA iko mkoani Arusha kuanzia Novemba 27, 2023 kutoa elimu ya Miliki Ubunifu kwa wafanyabiashara ambapo elimu hiyo imekwishatolewa kwa wafanyabiashara 182 wa Arusha Jiji, Halmashauri ya Wilaya Arusha, Meru na Longido.