Karibu katika tovuti hii ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA). Katika tovuti hii utapata taarifa kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA, njia za mawasiliano, mitandao yetu ya kijamii, taarifa na matukio mbalimbali yanayotokea katika Taasisi hii. Lengo ni kuhakikisha kuwa taarifa zote muhimu zinazohitajika zinapatikana katika tovuti hii ili kukuwezesha kuwa na uelewa mpana wa majukumu na huduma zitolewazo na BRELA.
Majukumu ya BRELA ni pamoja na kusajili Makampuni, Majina ya Biashara, Alama za Biashara na Huduma, Viwanda vidogo, kutoa Hataza, Leseni za Biashara kundi A na Leseni za Viwanda. Menejimenti na Wafanyakazi wa BRELA, wapo tayari kukusikiliza na kutoa huduma bora ili kufanikisha lengo lako.
Kwa kuwa utoaji wa huduma umeboreshwa kwa kutumia mifumo ya usajili kwa njia ya mtandao kupitia Online Registration System (ORS) na utoaji wa Leseni za Biashara kupitia Tanzania National Business Portal (TNBP), tunawasihi wateja wetu wote kutunza kwa usiri mkubwa taarifa zao za akaunti zinazotumika katika mifumo (jina la mtumiaji na neno la siri) kwa kuwa taarifa hizo zitaendelea kutumika katika huduma za sajili na leseni zinazofuata. Pale inapotokea mtu mwingine mbali ya mmiliki mwenyewe amehusika katika mchakato, mmiliki wa biashara anapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato huo na kupatiwa taarifa zote zinazohusu akaunti hiyo.
Ni matumaini yangu kwamba tovuti hii itasaidia upatikanaji wa taarifa zote zinazohitajika katika kukuwezesha kurasimisha biashara yako. Endapo hautapata taarifa unazohitaji, tafadhali usisite kuwasiliana nasi kupitia namba zetu za simu, barua pepe, mitandao ya kijamii au kufika katika ofisi za BRELA zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Mtwara.
Karibu sana katika tovuti hii ili uweze kurasimisha biashara yako kwani kwa kufanya hivyo utaondokana na vikwazo mbalimbali vya kibiashara na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu.