Habari
BRELA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA MAAFISA BIASHARA NCHINI
BRELA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA MAAFISA BIASHARA NCHINI
Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA) inaendeleza ushirikiano na maafisa nchini kwa kuwajengea uelewa na uwezo kuhusu huduma zinazotewa na BRELA ili waweze kuwasaidia wafanyabiashara kupata huduma hizo katika maeneo yao kwa urahisi, kwa kuzingatia kuwa maafisa hao wapo karibu zaidi na wafanyabiashara.
Kauli hiyo imetolewa na Bw Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA alipokuwa akitoa neno la ukaribisho katika ufunguzi wa kikao kazi cha pili kati ya Wakuu wa Idara na Sehemu za Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Bw Nyaisa ameeleza kuwa Serikali imekuwa na dhamira njema katika kuimarisha uratibu wa masuala ya viwanda, biashara na uwekezaji ambapo mwaka 2022 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliridhia kuanzishwa kwa Sehemu na Idara mpya ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini.
“Tunatambua kuwa bado kuna changamoto katika utekelezaji wa majukumu hayo kwa kiwango kikubwa, maafisa biashara wameendelea kutekeleza majukumu yao kwa mazoea, wakihusishwa zaidi na ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya biashara, masoko, minada, na nyumba za kulala wageni badala ya kutumika kama watoa huduma za msaada, ushauri, na uhamasishaji kwa wafanyabiashara na wawekezaji katika maeneo yao ya kazi” amesema Bw Nyaisa.
Katika kuhamasisha utendaji bora kwa maafisa biashara na kuwajengea hamasa
ya kazi, BRELA inatarajia kuanzisha utaratibu wa kutoa tuzo kwa maafisa biashara watakaofanya vizuri zaidi katika kurasimisha biashara katika maeneo yao. Vigezo muhimu vya kupima utendaji kazi wao vitaandaliwa ili kuwezesha uwazi na haki katika upatikanaji washindi.
Nyaisa, amesisitiza pia umuhimu wa maafisa biashara kuanzisha chama cha kitaaluma cha wataalamu wa biashara nchini kama ilivyo katika kada nyingine ili kuboresha ushirikiano na kusimamia viwango vya taaluma katika kada hii muhimu katika uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.
Ameendelea kueleza kuwa katika kuongeza ufanisi na kuboresha huduma, BRELA iko katika hatua za mwisho za kukamilisha maboresho ya mfumo wa Usajili (ORS) ili kuwezesha huduma zote zinazotolewa na BRELA kupatikana katika mfumo mmoja. Kukamilika kwa maboresho hayo kutawezesha utoaji wa huduma za leseni za biashara kundi “A” na “B” katika mfumo mmoja. Hatua hii itapunguza gharama na usumbufu kwa wafanyabiashara wetu na inaenda kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Kauli mbiu ya kikao kazi ni kukuza ushirikiano kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Taasisi za Uwezeshaji kwa Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Biashara, lengo ikiwa ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa Taasisi za Serikali na kufanya kazi kwa pamoja katika kuwahudumia wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla