Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

BRELA YASISITIZA ULINZI WA MILIKI UBUNIFU KUINUA UCHUMI WA VIJANA KUELEKEA DIRA 2050


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kupitia kikao cha ufuatiliaji na uendelezaji wa bunifu za wabunifu vijana kilichofanyika leo tarehe 27 Agosti 2026 Jijini Dodoma, imesisitiza kuwa ni muhimu kulinda haki za Miliki Ubunifu ili ziendelee kutumika kama nguzo kuu itakayoinua uchumi wa vijana na kuwezesha taifa kufikia malengo ya Dira 2050.

Akizungumza wakati wa kikao hicho cha kufuatilia bunifu za wabunifu vijana nchini kwa lengo la kupata taarifa za moja kwa moja kuhusu hatua ambazo kila mbunifu amefikia tangu ubunifu wake upate ulinzi wa Hataza, Afisa Sheria wa BRELA Bw. Calvin Rwambogo, alieleza kuwa ili vijana waweze kujikomboa kiuchumi na kuchangia Dira 2050 ni lazima wabaini, waendeleze na kuzilinda bunifu zao.

"Lengo la BRELA ni kuhakikisha wabunifu hawa tunawajengea uwezo kubaini, kuendeleza na kulinda bunifu zao, lakini tunataka pia kuwawezesha kutumia na kunufaika kikamilifu na haki za Miliki Ubunifu zinazotokana na kazi zao ili ubunifu uwe na tija na mchango wa kiuchumi kwao na kwa taifa zima." alisema Rwambogo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji wa Teknolojia (CDTT) katika Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Erasto Mlyuka aliipongeza BRELA kwa kuanzisha program hiyo ya kufuatilia bunifu za wabunifu vijana huku akiwataka wabunifu hao kutambua kuwa ubunifu ni mali kama mali zingine hivyo wanapaswa kuwekeza kimkakati katika bunifu zao.

Nao baadhi ya wabunifu walioshiriki kiako hicho walibainisha kuwa ufuatiliaji huo ni hatua muhimu ya kupata elimu zaidi ya kuendeleza bunifu zao na fursa ya kubaini changamoto zinazowakabili wakati wa kuziendeleza na kuzibiasharisha bunifu zao pamoja na kujadili aina ya msaada wanaohitaji kutoka taasisi wezeshi kama BRELA na wadau wengine. 

“Kati ya vitu vikubwa vinavyosaidia kuongeza ajira nchini ni viwanda vya uzalishaji bidhaa, ili kufikia kufikia Dira 2050 na kuongeza uzalishaji wa ndani tunahitajhi bunifu nyingi sana za wabunifu vijana waliopata nafasi kwenye programu kama hizi zilizoanzishwa na BRELA, rai yangu ziwafikie vijana ambao wako vijijini ili tuwapate watu watakaosaidia kuongeza uzalishaji kwenye viwanda na ajira kwa jamii” alisema Bw. David Dennis. 

Kikao hicho cha siku mbili ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya BRELA kuwalea wabunifu ili kuwajengea uwezo vijana katika kubaini, kuendeleza na kulinda bunifu zao na kuwawezesha kutumia na kunufaika na haki za Miliki Ubunifu.