Habari
BRELA YAIMARISHA URASIMISHAJI BIASHARA SEKTA YA UJENZI
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeshiriki katika Maonesho ya Wakandarasi yanayofanyika katika viwanja vya Lugalo Upanga Jijini Dar es Salaam leo tarehe 13 Agosti 2026,
Akizungumza katika maonesho hayo Msaidizi wa Usajili kutoka BRELA , Bi. Neema Shirima alisema lengo la Wakala kushiriki katika maonesho hayo ni kutoa huduma za papo kwa papo pamoja na elimu juu ya urasimishaji biashara kupitia mfumo ulioborehswa wa BRELA Online System (BOS).
“Kuendesha biashara katika mfumo rasmi kunamsaidia mdau kupata ulinzi wa kisheria pamoja na kupata fursa mbalimbali ikiwemo uwekezaji na mikopo kutoka taasisi za kifedha na uaminifu kwa wateja wao” Alisema Bi. Neema Shirima.
Aidha, Bi. Neema Shirima alitoa wito kwa wakandarasi, wajasiriamali, wafanyabiashara pamoja na wadau wote kwa ujumla kuendelea kutembelea banda la BRELA katika maonesho hayo ili kupata huduma za papo kwa papo pamoja na fursa ya kurasimisha biashara zao.
Nao baadhi ya wadau waliotembelea banda la BRELA waliipongeza Wakala kwa kuboresha huduma kupitia mfumo wa usajili na kusogeza huduma karibu katika maonesho hayo kwani imewasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za usajili wa majina ya biashara na kampuni papo kwa papo.
Ushiriki wa BRELA katika maonesho haya ni sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kuwasogezea huduma wananchi na kuwahamasisha wadau wakiwemo wa sekta ya ujenzi kupata fursa ya kurasimisha biashara zao.
Maonesho ya wakandarasi yanafanyika kwa siku 2 kuanzia leo tarehe 13 Agosti 2026 na kuisha 14 Agosti 2026. Hivyo BRELA itaendelea kushiriki katika maonesho hayo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi hatua ambayo itapelekea kuongezeka kwa uboreshwaji wa huduma za kijamii nchini.
