Habari
BRELA YATOA ELIMU YA URASIMISHAJI WA BIASHARA KWA WABUNIFU WA IFM
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa elimu kuhusu usajili wa majina ya biashara na kampuni, pamoja na ulinzi wa haki miliki kwa wabunifu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), jijini Dar es Salaam.
Elimu hiyo imetolewa Novemba 25, 2026, katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uwezo wanafunzi kuhusu urasimishaji wa biashara na umuhimu wa kulinda bunifu na utambulisho wa biashara zao.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Sheria wa BRELA, Bw. Calvin Lwambogo, ametoa elimu kuhusu ulinzi wa hataza, alama za biashara na huduma, akieleza umuhimu wa kulinda bunifu na utambulisho wa bidhaa au huduma ili kuongeza thamani na uwezo wa kushindana katika soko.
“Ulinzi wa hataza na alama za biashara ni muhimu katika kuhakikisha wabunifu na wafanyabiashara wanalinda haki zao za ubunifu dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa. Tunawahimiza vijana kutumia huduma za BRELA kusajili na kulinda bunifu zao ili ziweze kuwa na thamani na kuchangia maendeleo ya kiuchumi,” amesema Bw. Calvin Lwambogo.
Kwa upande wake, Afisa Usajili wa BRELA, Bw. Johnson Mmari, ametoa elimu kuhusu taratibu za usajili wa majina ya biashara na kampuni, huku akisisitiza umuhimu wa kurasimisha shughuli za biashara kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.
“Usajili wa jina la biashara na kampuni ni hatua muhimu katika safari ya ukuaji wa biashara. Tunawashauri vijana wenye mawazo ya kibiashara kuhakikisha wanarasimisha shughuli zao kupitia BRELA ili kujenga uaminifu, kutambulika kisheria na kutumia fursa mbalimbali za kibiashara,” amesema Bw. Johnson Mmari.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Bi.Yuneth George Thomas, Mhadhiri kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), ameipongeza BRELA kwa kutoa elimu hiyo, akieleza kuwa imewasaidia washiriki kupata uelewa zaidi kuhusu urasimishaji wa biashara na ulinzi wa haki miliki.
“Tunawapongeza BRELA kwa kuja kutoa elimu hii ambayo imetuwezesha kupata uelewa zaidi kuhusu usajili wa majina ya biashara, kampuni na ulinzi wa haki miliki. Elimu hii ni muhimu kwa wabunifu kwani inatupa mwanga wa namna ya kuanzisha biashara zetu kwa kufuata taratibu za kisheria, kulinda bunifu zetu na kujiandaa kutumia fursa za ujasiriamali baada ya masomo. Tunatarajia kuendelea kupata elimu ya aina hii ili kuongeza uelewa na uwezo wetu katika kujenga biashara endelevu,” amesema Bi Yuneth George Thomas.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za BRELA za kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, hususan vijana na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala na kuwahamasisha kuzitumia katika kurasimisha na kukuza shughuli zao za kibiashara.
