Habari
URASIMISHAJI WA BIASHARA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI KWA VIJANA ARUSHA
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeshiriki katika Jukwaa la Uwekezaji la Vijana 2026, lililoandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kupitia Youth Investment Club, kwa kushirikiana na Save Youth’s Dreams Foundation (SYDF) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA). Ushiriki huo umelenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu umuhimu wa urasimishaji wa biashara na namna unavyofungua fursa mbalimbali za uwekezaji nchini.
Jukwaa hili limefunguliwa Novemba 26, 2026, katika ukumbi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na litafanyika kwa siku tatu likiwakutanisha wanafunzi wa chuo hicho. Kupitia mafunzo haya, wanafunzi watajifunza kuhusu urasimishaji wa biashara, faida zake, na jinsi wanavyoweza kutumia fursa za biashara rasmi kukuza uchumi na uwekezaji wao.
Akizungumza katika jukwaa hilo wakati akitoa elimu kuhusu umuhimu wa urasimishaji wa biashara, Msajili Msaidizi Mwandamizi wa BRELA, Bi. Neema Kitala, amewaeleza vijana namna wanavyoweza kusajili na kurasimisha biashara zao kidijitali kupitia mifumo ya BRELA, bila kulazimika kufika ofisini.
“BRELA tumeboresha mfumo wetu ambao unaruhusu mtu kufanya au kutuma maombi yake akiwa sehemu yoyote kupitia mfumo wa BRELA Online Services (BOS), ambapo anaweza kutuma maombi ya usajili wa kampuni, usajili wa jina la biashara, maombi ya leseni ya biashara Kundi A pamoja na maombi ya leseni ya kiwanda na cheti cha usajili kwa kiwanda kidogo. Aidha, maombi ya usajili wa Alama za Biashara na Huduma pamoja na Hataza yanaweza kufanyika kupitia mfumo wa Online Registration System (ORS),” Alisema Bi. Kitala.
Bi. Kitala alisisitiza umuhimu wa vijana, hususan wanafunzi wa vyuoni, kuelewa taratibu za kuwasilisha maombi ya Hataza kwa ajili ya kulinda bunifu zao, akibainisha kuwa maombi hayo yanahitaji kuzingatia vigezo muhimu, ikiwemo ubunifu kuwa mpya, kuonesha hatua ya kibunifu na kuwa na matumizi ya kiutendaji.
“Ili kupata cheti cha Hataza, uvumbuzi lazima uwe mpya, uwe na hatua ya kibunifu na uweze kutatua changamoto katika jamii. Hata hivyo, baadhi ya maombi tunayopokea hayakidhi vigezo hivyo, ndiyo maana tumekuja kutoa elimu ili kuwasaidia vijana kuwasilisha maombi sahihi na kulinda bunifu zao,” Alisema Bi. Kitala.
Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi walioshiriki katika jukwaa hilo wameeleza kuwa awali hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na BRELA, lakini kupitia elimu hiyo wamefahamu umuhimu wa urasimishaji wa biashara pamoja na namna ya kulinda bunifu zao.
BRELA itaendelea kushiriki katika jukwaa hilo kwa siku tatu kuanzia Novemba 26 hadi 28, 2026 kwa kutoa elimu na huduma saidizi za usajili na leseni kwa wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
