Habari
JAFO: TANZANIA YAFIKIA VIWANDA 80,128, MAFANIKIO YA DIPLOMASIA YA UCHUMI YA RAIS SAMIA
JAFO: TANZANIA YAFIKIA VIWANDA 80,128, MAFANIKIO YA DIPLOMASIA YA UCHUMI YA RAIS SAMIA
Tanzania imefikisha jumla ya viwanda 80,128 hadi sasa, kutoka viwanda 50,000 vilivyokuwepo mwaka 2020, ikiwa ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia diplomasia ya uchumi inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa leo Juni 30, 2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jafo, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Maafisa Biashara, Uwekezaji na Viwanda uliofanyika jijini Morogoro. Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya wizara na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
“Nawapongeza maafisa biashara wote kwa kazi kubwa mnayoifanya katika halmashauri zenu. Mafanikio haya ya ongezeko la viwanda zaidi ya 30,000 yasingewezekana bila mchango wenu wa kusimamia kwa karibu maeneo yenu, kushirikiana na BRELA, na kuwa kiunganishi kati ya serikali na wajasiriamali,” alisema Dkt. Jafo.
Alieleza kuwa sekta ya viwanda na biashara imekuwa sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi wa nchi, ambapo sasa bidhaa nyingi zinazalishwa nchini na nyingine zinasafirishwa kwenda nje ya nchi. Alitaja bidhaa kama mchele kutoka Morogoro unaouzwa Senegal, mahindi yanayouzwa Uganda, Kenya na South Sudan, na bidhaa za viwandani kama vioo na gypsum zinazouzwa Kenya na Burundi.
Katika sekta ya chuma, Waziri Jafo alisema Tanzania sasa ina viwanda 24 vya kuzalisha nondo, ambapo baadhi ya miradi mikubwa kama ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) hutumia nondo za ndani pekee, na baadhi ya bidhaa hizo husafirishwa hadi DRC Congo na Burundi.
Kwa upande wa sukari, alisema uzalishaji umeongezeka kwa kasi, ambapo viwanda kama Kilombero Sugar vimeongeza uwezo wa uzalishaji kutoka tani 130,000 hadi kufikia zaidi ya tani 270,000 kwa mwaka baada ya upanuzi wa mitambo. Alisema hadi kufikia mwaka 2027, Tanzania itazalisha sukari ya kutosha kuliko mahitaji na kuanza kuuza nje.
“Katika cement, tulikuwa tunaagiza kutoka nje, lakini leo tuna viwanda vingi na uzalishaji umefikia tani milioni 10 kwa mwaka dhidi ya mahitaji ya tani milioni 8. Tuna akiba ya tani milioni 2 tunazouza nje,” aliongeza.
Aidha, Dkt. Jafo alisisitiza kuwa mchango wa biashara kwenye Pato la Taifa ni asilimia 4 na wa viwanda ni asilimia 7.3, hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufikia angalau asilimia 10 kwa kila sekta. Aliwataka maafisa biashara kujitathmini na kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa weledi na ubunifu.
“Mkutano huu ni fursa ya kufanya tathmini ya pamoja. Pia nawakumbusha kusimamia kwa uadilifu biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa pekee. Hili ni jambo muhimu kwa ulinzi wa soko la ndani,” alisisitiza.
Mkutano huo umehudhuriwa na maafisa biashara kutoka mikoa yote, wakuu wa taasisi, na wawakilishi wa sekta binafsi, na umelenga kuboresha utendaji wa maafisa hao katika kuimarisha biashara na uwekezaji nchini.