Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

RC TANGA AIPONGEZA BRELA


 

RC TANGA AIPONGEZA BRELA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi. Dkt. Batilda Salha Burian, ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa kazi za uboreshaji miundombinu ya utumiaji wa mfumo wa Usajili kwa njia ya mtandao (ORS), ambao umewezesha kuwafikia wafanyabiashara wengi na kukuza uchumi wa nchi leo tarehe 03 Juni 2024 Jijini Tanga.


Mhe. Balozi Dkt.Burian ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la BRELA katika maonesho ya Biashara ya 11 ya Utalii-Tanga Trade Fair 2024 yanayofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Usagala Jijini Tanga na kupata maelezo kuhusu majukumu na mchango wa Taasisi hiyo katika kuboresha mazingira ya biashara nchini.


“Naomba mzidi kuwa mabalozi wazuri na msisite kutoa elimu zaidi ya kuwaleta sehemu moja wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, ili kuongeza kasi ya uwekezaji pamoja na kukuza pato la Taifa na kuinua uchumi wa nchini”, amesisitiza Mhe. Dkt.Batilda.


Akiwa katika banda la BRELA, Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga alipokelewa na kupewa maelezo mafupi na Afisa Usajili wa wakala hiyo Bi. Julieth Kiwelu ambapo alimueleza kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo sambamba na jukumu la kusimamia sheria za Usajili wa Majina ya Biashara, Kampuni, Usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza na kutoa Leseni za Biashara kundi A, kutoa Leseni za Viwanda na kusajili Viwanda vidogo kwaajili ya kusaidia jitihada za Serikali za kuboresha ukuaji wa Uchumi.


BRELA imekuwa miongoni mwa taasisi za Serikali zinazoshiriki maonesho ya 11 ya Biashara na Utalii Tanga Trade Fair -2024 yaliyoanza tarehe 28 Mei,2024 na yanatarajia kufungwa ramsi tarehe 6 Juni 2024 Jijini Tanga ambapo mamia ya wananchi wamekuwa wakihudhuria katika viwanja hivyo kwa ajili ya kupata elimu kuhusu huduma zitolewazo na BRELA.


Maonesho hayo ambayo yamendaliwa chini ya Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na yamehusisha Taasisi mbalimbali za masuala ya Biashara ambapo yameongozwa na kauli mbiu, “Kuchochea Uwekezaji na Biashara kwa Uchumi Endelevu