Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

URASIMISHAJI WA BIASHARA NI MSINGI WA KILIMO CHENYE TIJA


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewahimiza vijana wanaoshiriki mpango wa Building a Better Tomorrow (BBT) kutumia fursa ya urasimishaji wa biashara ili kuongeza thamani ya shughuli zao za kilimo na ufugaji, hatua itakayowawezesha kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa.

Wito huo umetolewa Agosti 6, 2026 jijini Dodoma na Afisa Usajili kutoka BRELA Bw. Yusuph Mwasakafyuka, alipokuwa akitoa mafunzo ya urasimishaji biashara kwa vijana wa BBT wanaoshiriki Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni.

"Urasimishaji wa biashara ni nguzo muhimu itakayowajengea uwezo wa kufanya kilimo cha kisasa kinachozalisha tija badala ya kuendelea na mifumo ya jadi isiyo na ushindani wa kibiashara, ni hatua muhimu ya kujenga biashara endelevu zinazoweza kukua na kushindana." alisema Bw. Mwasakafyuka.

Aidha, Bw. Mwasakafyuka alibainisha kuwa elimu hiyo inalenga kuwahamasisha vijana kuanza mapema urasimishaji wa biashara ili wanapohitimu mafunzo na kuingia kwenye uzalishaji wa kibiashara wawe tayari kushiriki katika uchumi rasmi, kupata mikopo, masoko na fursa zinazotolewa na taasisi za kifedha.

Kwa upanade wake Msaidizi wa Usajili Mkuu, Bw. Nassoro Mtavu, aliwataka vijana hao kutambua umuhimu wa kusajili Alama za Biashara na kulinda bunifu zao akibainisha kuwa ulinzi wa haki za ubunifu huwapa wajasiriamali nafasi ya kunufaika na kazi zao, kuvutia uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mafunzo hayo ni muendelezo wa mkakati endelevu wa BRELA kuyafikia makundi yote ya wafanyabiashara ikiwemo vijana na kuwapa elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo ikiwemo usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Kampuni, Usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza, Utoaji wa Leseni za Biashara Kundi A pamoja na Leseni ya Kiwanda na Cheti cha Usajili wa Kiwanda kwa kiwanda kidogo.