Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

BRELA, COSOTA ZAWAKUMBUSHA THAMANI YA UBUNIFU TASUBA


BRELA, COSOTA ZAWAKUMBUSHA THAMANI YA UBUNIFU TASUBA.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Chama cha Hakimiliki na Haki Shiriki Tanzania (COSOTA), Tarehe 14 Mei 2025, zimetoa Mafunzo Maalumu kwa wasanii wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) juu ya Umuhimu wa kulinda kazi zao za Sanaa.

Katika mafunzo hayo, wasanii chipukizi wa TASUBA wamekumbushwa umuhimu mkubwa wa kusajili bunifu na kazi zao za sanaa, ikiwemo muziki, uchoraji, maigizo, filamu, na maandishi. BRELA na COSOTA wameeleza kuwa ubunifu ni mali halali ya msanii, na usiposajiliwa, mtu mwingine anaweza kuunufaika bila ridhaa yako.

"Msisubiri mjulikane ndipo msajili kazi zenu. Hakimiliki huanza pale ubunifu unapozaliwa – mnapaswa kuulinda mapema," alisisitiza Bw. Hashimu Rukwere wa COSOTA.

Kwa upande wake, Bw. Abdurikalim Nzori alieleza kwa kina kuhusu BRELA na namna ya kulinda kazi ya ubunifu, ili kuanzisha biashara ya sanaa inayoaminika na kulindwa kisheria.

Akisisitiza umuhimu wa miliki ubunifu, Bw. Nzori alisema “Miliki ubunifu ni mali halali kama mali nyingine — tofauti ni kwamba haishikiki kwa mkono, lakini ina thamani kubwa. Usiiache bila usajili, kwani inaweza kuibwa na kutumiwa na wengine bila faida yoyote kwako.”

Naye Perpetual Katondo, Meneja Huduma Saidizi za Taaluma TASUBA amesema Taasisi inaendelea kuthibitisha kuwa si tu kituo cha kukuza vipaji, bali pia nguzo ya maarifa na ulinzi wa kazi za wasanii. Mafunzo haya yamefungua macho ya wengi kuhusu thamani ya kulinda kazi zao kabla hazijaibwa au kutumiwa kinyume na matakwa yao.

Mafunzo haya ya leo yamekuwa kumbusho muhimu kwa wanafunzi wa TASUBA kuwa ubunifu una thamani kubwa na unastahili kulindwa, kuthaminiwa, na kuendelezwa. Katika dunia ya leo ambapo sanaa inakuwa chanzo kikuu cha ajira na utambulisho, ni muhimu kwa kila msanii kuelewa haki zake na hatua za kuchukua ili kulinda kazi yake.

Kauli mbiu ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani mwaka huu inayosema: “Miliki Ubunifu na Miziki – Sikiliza Mdundo wa Miliki Ubunifu” inawakumbusha wasanii kuwa si kila mdundo ni burudani tu, bali ni mali halisi ya ubunifu inayoweza kuwa chanzo cha mapato na urithi wa kudumu.