Habari
BRELA KUENDELEA KUWA KINARA WA URASIMISHAJI BIASHARA NCHINI
Waziri Kapinga ameyasema hayo Machi 04, 2026 jijini Mwanza wakati akifungua kikao cha pili cha Baraza la Wafanyakazi wa BRELA ambapo alibanisha kuwa ni muhimu kuwekeza kwenye mifumo iliyoboreshwa ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
“Matumizi ya mifumo inaweza kupunguza gharama za kiutawala kwa zaidi ya asilimia 25% hadi 30% na inasaidia kupunguza gharama za matumizi, ni lazima tuipime mifumo yetu dhidi ya gharama za matumizi,” alisema Waziri Kapinga.
Aidha, Mhe. Kapinga pia alieleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidigitali iliyoboreshwa inasaidia kuongeza urasimishaji wa biashara kwani wafanyabiashara wengi wanavutiwa kusajili biashara zao pindi huduma zinapopatikana kwa urahisi kupitia mifumo.
Vilevile Mhe. Kapinga aliongeza kuwa Tanzania inaweza kushuhudia uwepo wa biashara mpya kwa asilimia 20% mpaka 30% ndani ya miaka michache ijayo kutokana na namna ambavyo mifumo ya BRELA inaendelea kuboreshwa kimkakati zaidi.
“BRELA ni taasisi ya Kimkakati katika usanifu wa Uchumi wa Taifa na BRELA ndio lango la mafanikio ya biashara nchini kwahiyo ufanisi wa BRELA ni mojawapo ya hatua muhimu ya kufanikisha uendelevu wa biashara nchini Wizara tunajivunia kupitia BRELA, tumeona mafanikio kwenye ongezeko la usajili wa majina ya biashara, kampuni, alama za biashara na huduma pamoja na utoaji wa Leseni za Viwanda na Biashara” aliongeza Waziri Kapinga.
Awali akimkaribiasha Waziri wa Viwanda na Biashara kufungua kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa alisema katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2025/2026 Wakala imeendelea kuwa na mwenendo mzuri wa kiutendaji na kifedha ambapo taarifa inaonyesha utekelezaji wa malengo umefikia asilimia 78%.
