Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

"BRELA NA HALMASHAURI ZISHIRIKIANE KUTOA HUDUMA BORA"


 

"BRELA NA HALMASHAURI ZISHIRIKIANE KUTOA HUDUMA BORA"

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed leo Mei 12, 2023 ameeleza kuwa ni vyema Halmashauri na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kushirikiana katika kuboresha utoaji wa huduma za Leseni.

Amebainisha hayo wakati akifunga mafunzo ya siku
tatu ya Maafisa Biashara kutoka katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, kwenye Ukumbi wa Boma mkoani Mtwara.

Amesema kuwa jukumu mojawapo la kisheria la BRELA ni utoaji wa Leseni za Biashara kundi “A” kama ilivyo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) Tanzania Bara, ambazo kwa kupitia Sheria hiyo hiyo ya Leseni za Biashara zinatoa Leseni za Biashara kundi “B”, hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa ukaribu.

“Kwakuwa Sheria ya Leseni za Biashara inasimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka hizi mbili yaani BRELA na Halmashauri, kuna umuhimu wa Mamlaka hizi mbili kufanya kazi kwa ukaribu na kwa kuelewana na kushauriana njia bora za kuboresha utoaji wa huduma za Leseni na kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara wetu na hivyo kuongeza wigo wa walipa kodi, kuongezeka kwa ajira na ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ujumla wake”, amefafanua Mhe. Kanali Ahmed.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, Mkuu wa Sehemu ya Leseni za Biashara, Bw. Tawi Kilumile ameeleza kuwa ana matarajio ni kwamba Maafisa Biashara watakuwa Mabalozi wazuri kwa maafisa wengine.

“Katika mikakati ya BRELA kutumia rasilimali za Taifa vizuri na kwa pamoja, BRELA imeona kuna umuhimu wa kufanya mafunzo haya ya kuwajengea uwezo Maafisa Biashara wa Mikoa na Halmashauri zote ili waweze kuielewa kiundani Sheria ya Leseni za Biashara (Sura 208) na Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda (Sura 46).

Hivyo, ni imani yangu kuwa mnakwenda kuwa mabalozi wazuri wa BRELA na Serikali kwa ujumla na kuwa mfano bora kwa Maafisa wengine katika utoaji wa huduma bora na wezeshi”, ameeleza Bw. Kilumile.

Maafisa Biashara kutoka Mikoa ya Lindi, Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam na Mtwara wamepata mafunzo ya siku tatu kuanzia Mei 10 hadi 12, 2023.