Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

BRELA YAFANYA KAGUZI ELIMISHI VIWANDANI KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imefanya zoezi la ukaguzi wa leseni katika viwanda mbalimbali jijini Dar es Salaam, likilenga kuweka mazingira rafiki ya uendeshaji biashara na uwekezaji kwa kuhakikisha uzingatiaji wa sheria.

Ukaguzi huo uliofanyika tarehe 25 Machi 2026 katika maeneo ya viwanda ya Mikocheni, Mabibo na Mbezi Beach umeenda sambamba na uhuishaji wa leseni zilizokwisha muda wake pamoja na utoaji wa elimu kwa wamiliki wa viwanda kuhusu taratibu sahihi za uendeshaji biashara.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Leseni kutoka BRELA, Bw. Koyan Abubakar, alisema ukaguzi huo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa taasisi wa kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao bila vikwazo, huku wakizingatia sheria na kanuni zilizopo.

“Tangu tulipoanza zoezi hili, limekuwa likiendelea vizuri. Lengo lake ni kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwa uhalali kwa kuhakikisha wanahuisha leseni zao kwa wakati, pamoja na kupata mwongozo wa moja kwa moja wa kutatua changamoto wanazokutana nazo,” alisema Bw. Koyan.

Aidha, alieleza kuwa BRELA imeimarisha utaratibu wa kufanya kaguzi hizo kwa kasi zaidi, ikilenga kufikia angalau viwanda vitano na biashara 10 kwa siku, hatua itakayowezesha kuwafikia wafanyabiashara wengi zaidi kwa muda mfupi.

Kwa upande wake, Meneja Msimamizi wa kampuni ya Speed Flex Company Ltd, Bw. Nyari Said Nkya, alisema kaguzi zinazofanywa na BRELA viwandani zimeleta unafuu mkubwa kwa wafanyabiashara.

“Huduma hizi kutufikia hapa kiwandani zinarahisisha mambo mengi. Tunapata ufafanuzi wa moja kwa moja, elimu ya matumizi sahihi ya leseni, pamoja na utatuzi wa changamoto zetu kwa haraka zaidi bila kulazimika kufuata huduma mbali,” alisema Bw. Nyari.

Zoezi la kaguzi elimishi viwandani ni mkakati endelevu wa BRELA unaolenga kuelimisha, kurasimisha biashara, kubaini na kutatua changamoto za wafanyabiashara, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda inayozingatia sheria na taratibu.