Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

BRELA YAPATA VIONGOZI WAPYA WA TAWI LA TUGHE


Katika uchaguzi huo uliofanyika tarehe 23 Februari 2025, wanachama wa TUGHE, tawi la BRELA walipiga kura kumchagua Mwenyekiti wa tawi na Katibu wake, Mwenyekiti wa Kamati ya wanawake na Katibu wake, Mwakilishi wa vijana na walemavu pamoja na wajumbe.

Uchaguzi ulikuwa na ushindani mkali katika nafasi ya uenyekiti wa tawi ukiwakutanisha wagombea wawili wenye ushawishi mkubwa ambao ni Bw. Andrew Malesi kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu na Bw. Francise Philimbi kutoka Kurugenzi ya Leseni za Viwanda.

Aidha, kufuatia ushindani huo na hesabu ya kura zilizopigwa na wanachama wote, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Sara Rwezahula alimtangaza Bw. Francise Philimbi kuwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 31 kati ya kura 51 zilizopigwa huku Bw. Andrew Malesi akipata kura 20 kati ya kura 51 zilizopigwa na wanachama wote.

Wengine walioibuka washindi katika uchaguzi huo ni Bi. Yvone Masele alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya wanawake kwa kupata kura 26 kati ya 30 zilizopigwa, Bi. Mgeni Shaban aliyeshinda nafasi ya Katibu wa Kamati ya wanawake kwa kupata kura 25 za ndio, kura 2 za hapana na moja iliharibika.

Kwa upande wa mwakilishi wa vijana, Bw. Ismail Masoud alishinda kwa kupata kura 48 za ndio huku kura 2 zikiwa za hapana na kwa upande wa mwakilishi wa walemavu Bi. Sophia Mtunzi alishinda kwa kupata kura 50 za ndio huku moja ikiwa ni hapana.

Awali akizungumza baada ya kutangaza washindi hao, Bi. Rwezahula alitoa rai kwa matawi mengine ya TUGHE ambayo yanaendelea na uchaguzi wa viongozi kuiga mfano wa tawi la BRELA kwa namna walivyoendesha uchaguzi kuanzia maandalizi mpaka mchakato wa kutangaza washindi.